• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Wezi wa nguo wanaojifanya maafisa wa Kenya Power

Wezi wa nguo wanaojifanya maafisa wa Kenya Power

NA RICHARD MAOSI

VISA vya wizi wa nguo zilizoanikiwa kwenye kamba baada ya kufuliwa ili kukauka vimeandikisha kuongezeka, hasa katika mitaa mbalimbali Kaunti ya Nairobi.

Kero hiyo, hata hivyo, inaathiri mitaa ya wenye mapato ya chini na ya kadri.

Aghalabu, hushuhudiwa msimu wa Krismasi unapokaribia na pia wakati wa kukaribisha mwaka mpya.

Wahuni wanaotekeleza uhalifu huo, wameibuka na ujanja – wanavalia mavazi rasmi ya Kampuni ya Usambazaji Nguvu za Umeme Nchini (KPLC) ni misheni yao isifichuke.

Aidha, wanasingizia kwamba wamekuja (kwenye ploti) kuangalia mita au kukata stima jambo ambalo limefanya kuwa vigumu kuwashuku.

Wanalenga mazulia, nguo na viatu nyakati za mchana wenye nyumba wanapokuwa wameenda kazini.

Wamekuwa wakianua nguo zilizofuliwa na kuanikwa kisha wanazijaza ndani ya gunia na hatimaye kuuza kama kifurushi cha mtumba katika soko maarufu la Gikomba.

“Zangu zilienda zikiendelea kumwaga maji,” anasema mkazi mmoja wa Ngara ambaye anajitambulisha kwa jina moja pekee, John.

Anasema siku moja alipokuwa nyumbani kwake alimwona mtu akinyatia kamba kisha akaanza kuanua nguo zake moja baada ya nyingine.

Mara ya kwanza, John alifikiria ni afisa wa Shirika la Umeme, kwa sababu alikuwa amevalia koti jeeupe lenye maandishi ya KPLC.

Ilibidi awaite majirani ambao walishirikiana na kumkamata, lakini mwizi aliponyoka walipokuwa wakimpeleka kwenye kituo cha polisi cha Central.

“Wakikutana na nguo hasa za watoto wanafagia kila kitu,” asema Kelvin Onganga kutoka mtaa wa South C.

Anasema anakoishi wapangaji wameamua kuongeza mlinzi wa mchana kwani wezi ni wengi nyakati za mchana kuliko usiku.

Ufichuzi wa Taifa Leo Dijitali, umebaini soko la nguo za watoto, akina dada, mishipi na viatu ni kubwa.

Biashara ya kuuza nguo za rejareja mitaani na hata katikati mwa jiji la Nairobi hupamba moto hasa ifikapo Desemba.

Viatu vya wanaume ambavyo madukani hugharimu kati ya Sh 3, 000 – 4, 000 utauziwa Sh500 hivi mitaani.

Mwaka uliopita, 2022 biashara ya mitumba nchini ilizua mjadala mkali, baadhi ya viongozi wakitaka ipuuziliwe mbali.

Hata hivyo, wafanyibiashara wengi walijitokeza mitandaoni kujitetea wakidai kwamba wanategemea kazi ya kuuza nguo za mitumba kujikimu kimaisha kwa sababu ya nafasi finyu za ajira zinazopatikana nchini.

Kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga, alinukuliwa akisema sekta hiyo haiwezi kufungwa kwa sababu inatoa ajira nyingi kwa Wakenya.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Sababu ya mibuyu kuhusishwa na mashetani

Serikali yalenga kukusanya Sh4.2 bilioni kila siku

T L