• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Al-Shabaab waua mwanamume kwa kukataa kuwaonyesha vituo vya maangamizi zaidi

Al-Shabaab waua mwanamume kwa kukataa kuwaonyesha vituo vya maangamizi zaidi

NA KALUME KAZUNGU

MTU mmoja ameuawa kinyama kwa kuchinjwa wakati Al-Shabaab wametekeleza mashambulio na kuteketeza nyumba tano kwenye kijiji cha Widho-Mashambani kilichoko Lamu Magharibi saa nane usiku wa kuamkia Jumatano.

Walioshuhudia wanasema magaidi zaidi ya 30 waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki na visu, walifika ghafla vijijini na kuanza kuvunja milango na kuingia ndani kwa lengo la kuwapata wanaume na kuwaua.

Pia wameiba mbuzi, unga, mahindi na hata wakachinja kuku kabla ya kuteketeza nyumba na kisha kutorokea msituni.

Aliyeuawa alitambuliwa kwa jina George Sumit Gitocho aliyekuwa na umri wa miaka 49.

Alikuwa baba wa watoto sita na alikuwa akihudumu kama bawabu wa Shule ya Msingi ya Majembeni, Lamu Magharibi.

Bi Eunice Mong’are, mama wa watoto sita na ambaye marehemu alichinjwa mbele ya mlango wake, anasema alisikia mlango ukigongwa usiku wa manane kabla ya magaidi kuuvunja na kuingia ndani.

Walimhoji na kuuliza aliko mumewe na akawaambia hakuwepo nyumbani kwani alikuwa safarini.

Kulingana na Bi Mong’are, magaidi hao ambao baadhi yao walijifunika nyuso zao walijitambulisha kama Al-Shabaab halisi, wakidai kutoka nchi jirani ya Somalia.

Bi Mong’are alikuwa na watoto wake watatu wa kiume wa umri wa miaka 13, 11 na mwingine mchanga wa miezi mitatu wakati magaidi walipovamia boma lake.

“Walifika nyumbani saa nane usiku. Walibisha mlangoni mara mbili na walipoona hawafunguliwi wakauvunja na kuingia ndani. Walinipata na wanangu watatu. Wakauliza aliko mume wangu lakini nikawaambia yuko safarini. Walituamuru mimi na watoto wangu kutoka nje na kulala chini. Punde tulipotoka hivi tukapata wakiwa wamemshika mjombangu Gitocho. Walituambia wao wametoka Somalia kuja kuua wanaume maeneo yetu kama njia ya kulipiza kisasi wakisema ‘serikali ya Kenya imeua watu wao nchini Somalia. Walimchinja mjombangu mbele yetu tukiona kabla ya kutuamuru kurudi ndani ya nyumba kulala. Mmoja akisisitiza kwamba wao wataendelea kuchinja wanaume vijijini mwetu hadi serikali ya Kenya isitishe kutumia nguvu nchini Somalia,” akasema Bi Mong’are.

Ameiomba serikali kuimarisha usalama vijijini mwao, akitaja kuwa wanaishi kwa hofu kufuatia mauaji ya kila mara maeneo yao.

“Tumeililia serikali kila mara kutujengea kambi za polisi na jeshi (KDF) maeneo haya lakini wapi. Tunahangaika kila wakati. Hatuna amani kabisa. Serikali isikie kilio chetu na ijenge kambi za walinda usalama huku,” akasema Bi Mong’are.

Taifa Leo pia imebaini kuwa mojawapo ya nyumba tano zilizochomwa na magaidi ni ya Askari wa Akiba (NPR) anayehudumu eneo hilo.

Afisa huyo alikuwa akiwa kwenye doria za usiku eneo la mbali kidogo magaidi walipofika kwake na kuteketeza nyumba yake, kuiba mbuzi, mahindi na vifaa vya kielektroniki.

Bw Simon Kariuki, mkazi wa Juhudi alisema ukosefu wa usalama umesababisha wengi wao kukosa kujiendeleza maishani wakifikiria hatima yao ya maisha.

“Huwezi hata kutulia na kujiendeleza ikiwemo kujenga nyumba ya kudumu eneo hili. Hofu iko tele. Wakazi hawalali tena mabomani mwao. Wengi kila jioni hukimbilia kambi ya wakimbizi katika Shule ya Msingi ya Juhudi huku wengine wakilala vichakani kwa kuhofia kulengwa na hawa magaidi. Serikali itilie mkazo msako na kuwaangamiza hawa wahalifu wanaoua watu kila mara na kuiba mali,” akasema Bw Kariuki.

Mauaji ya Jumatano yanajiri wakati ambapo karibu familia 200 bado zinaishi kambini kwenye shule ya msingi ya Juhudi iliyoko Lamu Magharibi baada ya kuhama kutoka kwa makazi yao rasmi katika vijiji vya Juhudi, Salama, Widho, Marafa, Mashogoni na viungani mwake kwa kuhofia usalama wao.

Wiki tatu zilizopita, magaidi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab walivamia kambi ya Juhudi wakilenga kuwaua wanaoishi hapo lakini jaribio lao likatibuliwa na walinda usalama wanaolinda kambi hiyo. Uvamizi huo ulitekelezwa Agosti 24, 2023 majira ya saa tisa alfajiri.

Mnamo Agosti 22, 2023, magaidi wa Al-Shabaab walivamia magari ya wapitanjia eneo la Lango La Simba kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, ambako walimchinja dereva na msaidizi wake.

Hii ni baada ya jaribio lao la kuvamia kambi ya polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) eneo la Pandanguo, Lamu Magharibi kutibuliwa na walinda usalama kambini humo.

Agosti 21, 2023, magaidi wanaoshukiwa kuwa Al-Shabaab walivamia kijiji cha Salama usiku, ambapo waliteketeza nyumba nane na kanisa moja, wakaiba mbuzi na kuku na kuvuna mahindi mashambani kabla ya kujitoma kwenye msitu wa Boni.

Kati ya Juni na Septemba 2023, eneobunge la Lamu Magharibi limeshuhudia msururu wa mashambulio ya Al-Shabaab ambayo yameacha zaidi ya watu 20, raia na walinda usalama wakiuawa, huku nyumba zipatazo zaidi ya 20 ikiwemo kanisa, zikiteketezwa na magaidi hao.

Juma lililopita, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alifika katika eneo la Faza, ambapo aliahidi kuwa serikali itapambana vilivyo na kuhakikisha magaidi wa Al-Shabaab wameangamizwa kabisa Lamu na maeneo yote nchini.

  • Tags

You can share this post!

Maseneta wamkataza gavana kutengenezea mke wake ofisi

Sakaja atabasamu madiwani wa UDA wakiunga mkono...

T L