• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Atwoli atengwa vyama vikipinga mswada wa Ruto

Atwoli atengwa vyama vikipinga mswada wa Ruto

NA BENSON MATHEKA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini Kenya (COTU- K), Bw Francis Atwoli ametengwa na wafanyakazi kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023.

Upinzani dhidi ya mswada huo umekuwa ukiongezeka huku vyama vya wafanyakazi vilivyo chini ya Cotu vikijitenga na Bw Atwoli ambaye kwa mujibu wa wadhifa wake, anafaa kuwa akiwatetea wafanyakazi.

Mnamo Mei 8, Atwoli aliwakashifu watumishi wa umma na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa kupinga asilimia tatu ya ada ya nyumba iliyopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2023. Katika taarifa iliyotolewa mnamo Mei, Atwoli ilieleza kuwa masuala yanayohusu ada hiyo tayari yalijadiliwa katika mkutano kati ya Rais na viongozi wa vyama vya wafanyakazi.

“Inasikitisha kuwa hata baada ya Katibu Mkuu wa COTU (K) kuwaalika viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi na Rais wa Kenya kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali yakijumuisha Hazina ya Nyumba, waliosusia sasa wanalalamikia yaliyopitishwa katika mkutano huo,” COTU ilisema.

Lakini vyama vya wafanyakazi vinasisitiza kuwa havikushauriwa na ada iliyopendekezwa itaumiza wafanyakazi ambao tayari wamelemewa na gharama ya maisha.

“Mamlaka za ushuru zinaendelea kuwaelemea wafanyakazi katika sekta ya umma ambao mishahara yao inakatwa huku wakiwaacha nje walioajiriwa katika sekta ya kibinafsi,” Vyama vya Wafanyakazi vya Sekta ya Umma vilisema katika taarifa.

Vyama vya wafanyakazi pia vimeonya kuwa vitaitisha mgomo iwapo Bunge litapitisha ushuru ambao wafanyikazi wanahofia unaweza kupunguza mapato yao.

Mnamo Jumatatu, viongozi wa muungano huo walishikilia kuwa mswada huo ukipitishwa, makato yatawaelemea wafanyakazi.

Vyama ambavyo viliandamana ni pamoja na Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu vya Kenya (Kusu), Muungano wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (Uasu), Chama cha Madaktari wa Kenya na wataalamu wa Meno (KMPDU), Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) na Muungano wa Maafisa wa Kliniki wa Kenya (KUCO).

Vyama vya wafanyakazi vilisema wawakilishi wao hawakushauriwa wakati wa kutayarisha Mswada na kwamba watakubali tu mswada unaopendekeza hatua zinazolenga kupunguza mzigo wa kifedha kwenye mabega ya wafanyikazi wa Kenya.

“Kwa hivyo, tunakataa kuanzishwa kwa Ushuru wa Nyumba hadi mashauriano na mazungumzo sahihi na wawakilishi wa wafanyikazi yafanywe,” walisema.

Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Wasonga alionya kuwa wafanyakazi hawatakubali ada hiyo.

“Kwa hili, hatutawasaliti kwa kwenda Ikulu,” mwanaharakati huyo wa vyama vya wafanyakazi alisema.

Huku akiunga mkono mapendekezo ya ada ya nyumba, Atwoli aliunga mkono serikali akisema huo si ushuru bali “ni mpango mzuri wa kujenga nyumba za bei nafuu kwa wafanyikazi wa Kenya”.

Lakini vyama vya wafanyakazi vinasisitiza kuwa litakuwa pigo kwa wafanyakazi ambao watasalia bila mapato ya kukidhi mahitaji yao.

  • Tags

You can share this post!

Njaa kutesa Wakenya hadi 2024 – Ripoti

Thugge kuondoa sheria inayozuia Wakenya kuweka na kutoa kwa...

T L