NA RICHARD MAOSI
KATIBU Mkuu wa Muungano wa Kutetea Wafanyikazi Nchini (COTU) Francis Atwoli amejitetea dhidi ya shutuma za kusalia kimya, huku mishahara ya wafanyakazi ikinyanyaswa kwa ushuru mzito.
Amesema muungano huo uko imara kutetea wafanyakazi na amekashifu vyombo vya habari kwa kudai COTU ina utepetevu, wakati ambapo inapaswa kusimama kidete na wafanyakazi.
Atwoli ametaka Baraza la Wanahabari Nchini (MCK) kuwachukulia hatua kali kisheria asasi za habari zilizochapisha taarifa zake, “kwamba nimekunja mkia”.
Ameshikilia kuwa COTU ni muungamo wa pili mkubwa zaidi Afrika, wenye wanachama zaidi ya milioni nne na majukumu yake makubwa ni kuwakilisha wafanyakazi ndani na nje ya nchi.
“Tuna imani kubwa kwenye mazungumzo na maelewano ili kusitisha mizozo, lengo likiwa ni kuleta uwiano baina ya washikadau husika ikiwemo serikali, waajiiri na wafanyakazi,”Atwoli akasema.
Awali, Katibu huyo katika habari hii, https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/cotu-sasa-yatisha-kuitisha-mgomo-kupinga-ushuru alikuwa ametangaza kwamba sasa muungano huo utaitisha mgomo kuhusu ushuru unaosakama wananchi.
Aliungama huu ni wakati ambao taifa linapitia changamoto za hali ngumu ya uchumi, mfumuko wa bei na hali ngumu ya maisha, hivyo basi kama chama wamejizatiti kuboresha uchumi.
Alisema COTU inajituma kuhakikisha Wakenya hawapotezi ajira na pia kuandaa mazingira bora ya kufanikisha ukuaji wa uchumi ambao unazidi kudorora.
Kulingana na Atwoli, tangu kupitishwa Katiba ya 2010, COTU imeshiriki pakubwa katika mageuzi ya ukuaji wa viwanda.
“Msimamo wetu ni kuchochea mazungumzo na maelewano kama mbinu mwafaka ya kutatua migogoro badala ya kushiriki maandamano ambayo yamekuwa yakiwaumiza wanachama wetu,” akasema.
Amevitaka vyombo vya habari kutoa taarifa za kuaminika, hasa vinaporipoti kuhusu maslahi ya wafanyakazi na utendaji kazi.
Bw Atwoli, 2022 alikuwa akiunga mkono kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye kwa sasa ni mstaafu.
Hata hivyo, baada ya Bw Odinga kuonyeshwa kivumbi katika kinyang’anyiro cha urais, Atwoli baadaye aliunda urafiki na Rais wa sasa Dkt William Ruto.
Amekuwa akikosoa Raila Odinga kwa kuandaa maandamano, japo yalisitishwa kuruhusu mazungumzo.