• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Azimio wawaenzi waandamanaji waliouawa, kujeruhiwa na polisi

Azimio wawaenzi waandamanaji waliouawa, kujeruhiwa na polisi

NA WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amewaongoza wafuasi wa muungano huo kuwasha mishumaa na kuwaenzi waliopoteza maisha yao na waliojeruhiwa na maafisa wa polisi wakati wa maandamano ya kupinga kuongezwa kwa ushuru na kupanda kwa gharama ya maisha nchini.

Bw Odinga ametembelea Hospitali ya Mama Lucy Kibaki kabla ya kuelekea katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH). Akiwa katika Hospitali ya Mama Lucy, viongozi wa Azimio walioandamana naye Mbw Edwin Sifuna (Seneta wa Nairobi) na Otiende Amollo (mbunge wa Rarieda) wamewatembelea wagonjwa waliolazwa baada ya kujeruhiwa wakati wa maandamano.

Baadaye kiongozi wa Azimio anatarajiwa kuhutubu akiwa Lang’ata.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Bw Opiyo Wandayi amesema ni shughuli ya kuwaenzi walioangamia wakati wa maandamano ni muhimu ili pia kuzifariji familia zao.

“Tunalaani hatua ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa hawana hatia yoyote. Tunaendelea kuandaa orodha kamili ya waliopoteza maisha yao,” amesema Bw Wandayi.

Katika Kaunti ya Siaya, Gavana James Orengo, Spika wa Bunge la Kaunti ya Siaya George Okode, diwani wa Siaya Township Obiero Otare wamejitokeza wakiwa wamevaa mavazi meupe walipojiunga na wakazi kuwasha mishumaa katika Ahindi Gardens kuwapa heshima waandamanaji waliouawa na polisi wakati wa maandamano Siaya. Katika kaunti hiyo ambako ndiko nyumbani kwa Bw Odinga, watu watatu waliangamia baada ya kupigwa risasi.

Katika kaunti ya Kisumu ambayo inapakana na Siaya, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisumu Jack Oraro amejiunga na viongozi wengine katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga kuwaenzi raia waliouawa na polisi kwenye maandamano ya Azimio. Mbali na kuwasha mishumaa, wamebeba pia maua kwa ajili ya kuzifariji familia za ama walioaga dunia au waliojeruhiwa.

Shughuli kama hiyo pia imefanyika katika kaunti za Homa Bay, Kisii, Nakuru, na Mombasa miongoni mwa nyingine.

Misa ya kuwakumbuka waliouawa na polisi wakati wa maandamano ya Azimio ikiendelea katika Kanisa la Nakuru Christ the King. PICHA | BONIFACE MWANGI
  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Kwa kiongozi dikteta, mwisho wa ubaya ni aibu

Mwanawe Uhuru apinga serikali kumpokonya silaha

T L