NA MERCY KOSKEI
VIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya wamelalamikia kuhangaishwa kwa aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga.
Malalamishi yao yanayotokana na ripoti ya kutekwa nyara kwa Bw Njenga, maafisa wa polisi wakitajwa kuhusishwa na kupotea kwake.
Wakihutubia wanahabari jijini Nairobi mnamo Jumapili Septemba 17, 2023, viongozi hao walishutumu polisi kwa madai ya kumteka nyara ‘pasta’ Njenga.
Bw Njenga na msaidizi wake Felix Lakishe, wanasemekana kutekwa nyara na watu wasiojulikana Jumamosi usiku, Septemba 16, 2023 katika Kaunti ya Kiambu.
Wakiongozwa na Bi Martha Karua, viongozi hao walisema kuwa Bw Njenga alichukuliwa na maafisa wa polisi walaghai ambao hawakujitambulisha.
Bi Karua alitaja tukio hilo kama “utekaji nyara wa mtindo wa majambazi” huku akisikitika kuwa kufikia sasa maafisa wa polisi hawajakubali kuhusika na kupotea kwa Njenga.
Alidai kuwa ‘kutekwa nyara’ kwa Njenga “ni jaribio la kuvuruga Wakenya kutoka kwa fujo za kiuchumi ambazo serikali ya Kenya Kwanza imesababisha”.
“Tunasimama na familia ya Maina Njenga ambaye alitekwa nyara na polisi jana usiku. Tunalaani vikali kitendo hicho. Ilikuwa ni utekaji nyara wa mtindo wa majambazi. Polisi wamesema hawajui aliko,” Karua alisema.
Kiongozi huyo wa Narc – Kenya alidai mrengo wa Kenya Kwanza umeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi waliowachagua na kuwa inazidi kukata tamaa.
Alisema kuwa uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza utazidi kuwa wa kikatili na kidikteta, akiomba wananchi kupigana na kudai haki zao za kiraia na za kimsingi.
Kwa upande wake, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alikashifu tukio hilo akisema kuwa nchi hii iko chini ya utawala wa sheri, akiongeza kuwa kinachoshuhudiwa ni mabadiliko kamili ya mafanikio yote ambayo tumepata.
Bw Kalonzo alisema upinzani hautakubali matukio hayo na kuwa wanasimama kidete na familia ya Bw Njenga na Wakenya wote ambao haki zao zinalindwa na Katiba.
Bw Eugene Wamalwa, alisema kuwa Kenya Kwanza inakandamiza viongozi wa Azimio na wafuasi wake.
Awali, wakili Maina Njenga, Bw Ndegwa Njiru aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kisa hicho kilitokea saa tano usiku katika eneo la Banana, Kaunti ya Kiambu.
Watu wasiojulikana walifika na kutaka kuzungumza naye.
Kulingana na wakili Ndegwa, walivuta mteja wake na kumweka ndani ya gari lililokuwa na nambari ya usajili ya Sudan na kuondoka pamoja na msaidizi wake.
Bw Njiru alisema kuwa watu hao hawakujitambulisha wala kumpa sababu za kumkamata, akisema “waliwateka nyara na kuwapeleka eneo lisilojulikana”.
Kupotea kwake, kunajiri siku moja kabla ya kufikishwa kortini kufuatia kesi inayomkabili.