• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Bandari za Mombasa na Lamu zapata kreni za kielektroniki

Bandari za Mombasa na Lamu zapata kreni za kielektroniki

NA KALUME KAZUNGU

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Nchini (KPA) imenunua kreni tano za kisasa kupiga jeki shughuli ya kupakia na kupakua mizigo kwenye bandari za Lamu na Mombasa.

Kreni hizo zilizonunuliwa kutoka nchini Ujerumani, ziligharimu serikali kima cha zaidi ya Sh3.7 bilioni.

Mashine hizo tano zilisafirishwa na kufikishwa bandarini Lamu kupitia meli ya MV UHL Finesse.

Akizungumza wakati alipozipokea, Meneja wa Masuala ya Miradi ya Uhandisi na Upekuzi wa KPA, Felix Ong’wen alisema kreni tatu kati ya tano zitahudumu kwenye bandari ya Lamu huku mbili zikielekezwa kuhudumia bandari kuu ya Mombasa.

Bw Ong’wen alisema kuwasili kwa kreni hizo kama hatua mwafaka itakayosaidia kuharakisha upakiaji na upakuaji wa mizigo kuingia na kutoka kwenye meli, hasa katika bandari hizo mbili; Lamu na Mombasa.

“Ni kreni mpya na zinazofanya kazi kwa njia ya kielektroniki. Ni matarajio yetu kwamba kupitia vifaa hivi, shughuli za uchukuzi bandarini Lamu na Mombasa zitaimarika hata zaidi,” akasema Bw Ong’wen.

Meneja Mhandisi wa Uchukuzi wa Mizigo KPA Swaleh Karuwa, alisema anatarajia kampuni nyingi zinazoshughulika na uchukuzi kupitia meli kuvutiwa zaidi na huduma zinazotolewa kwenye Bandari ya Lamu na Mombasa kufuatia ununuzi wa kreni hizo za kisasa.

Kutoka kushoto, Meneja wa Masuala ya Miradi ya Uhandisi na Upekuzi wa KPA, Felix Ong’wen, mwenzake wa Uchukuzi wa Mizigo KPA Swaleh Karuwa na Mhandisi Mkarabati Mkuu katika Bandari ya Lamu, Joseph Nyachwaya baada ya kupokea kreni bandarini Lamu. Picha / KALUME KAZUNGU

Awali, bandari ya Lamu ilikuwa na kreni mbili pekee zinazotumia maji na ambazo zilikuwa zikitoa huduma japo kwa upole.

Kreni zilizokuwepo tayari zilikuwa zimetumika kwa karibu miaka mitano.

“Kreni tatu zitakazohudumia bandari ya Lamu na mbili zitakazotumika Mombasa zote ni mpya na za kielektroniki. Hii inamaanisha upakiaji na upakuaji wa mizigo utarahisishwa na kuharakishwa,” akasema Bw Karuwa.

Naye Mhandisi Mkarabati Mkuu katika Bandari ya Lamu, Joseph Nyachwaya alisema furaha yake ni kwamba kuwasili kwa kreni hizo tatu bandarini humo ni hatua kubwa itakayovutia meli zaidi kutia nanga bandarini Lamu.

“Tayari meli 22 zimetia nanga bandarini Lamu tangu kuzinduliwa kwake Mei 20, 2021. Ujio wa vifaa hivi leo ni kumaanisha biashara inapanuka zaidi hapa Bandari ya Lamu. Tunatarajia meli zaidi kufika hapa na huduma zinazotolewa kuharakishwa kwani kreni ni nyingi sasa,” akasema Bw Nyachwaya.

Bandari ya Lamu ambayo iligharimu serikali kima cha Sh310 bilioni kujengwa, inatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha biashara na uchukuzi wa meli kutoka Kenya hadi Ethiopia, Kusini mwa nchi ya Sudan na ukanda wa Afrika Mashariki kwa jumla.

Lamu ni bandari ya pili kubwa baada ya ile ya Kilindini Kaunti ya Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

Jackson Mutiso ashinda Sh20 milioni za SportPesa Midweek...

Asukumwa jela kwa kutishia kuua mamake

T L