• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Besigye amshambulia Rais Museveni kwa kukwamilia uongozini

Besigye amshambulia Rais Museveni kwa kukwamilia uongozini

NA WYCLIFFE NYABERI

KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amemsuta Rais ya nchi hiyo Yoweri Museveni kwa kukwamilia uongozini.

Besigye aidha amekosoa vikali hatua ya Bunge la Uganda kufanyia katiba ya nchi hiyo marekebisho ili kuondoa sharti kwamba wawaniaji wa urais wawe chini ya umri wa miaka 75.

Marekebisho hayo yalifanyika mwaka 2017 na kufuatia kupitishwa kwake Bungeni, Rais Museveni alipata fursa nyingine ya kuzidi kuwania urais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Bw Museveni amekuwa mamlakani tangu taifa hilo lijinyakulie uhuru wake.

Akizungumza mnano Desemba 3, 2023, alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa mbunge wa zamani wa Mugirango Magharibi, Benson Kegoro katika Kaunti ya Nyamira, Besigye alimpiga vijembe Museveni kwa kusema japo aliifanyia katiba mabadiliko ili kumpa nafasi kuzidi kutawala, hawezi kufanyia Bibilia mageuzi kwani kitabu hicho kitakatifu kinakadiria maisha ya binadamu ulimwenguni kuwa miaka 70.

“Huko kwetu kulikuwa na koma kwa miaka ambayo viongozi hawawezi kuwania urais tena wakizidi miaka 75. Hivi karibuni, ilifika kiongozi wetu akasema aah, iondolewe. Iliondolewa na haiko tena kwenye katiba. Lakini alisahau kwamba kuna koma iliyowekwa na Bibilia na Bibilia haiwezi ikabadilishwa. Ni katiba ambayo haiwezi ikabadilishwa,” Besigye akasema.

Mwanasiasa huyo ambaye amejaribu kuwania urais wa Uganda kwa safari nyingi bila mafanikio, alieleza mazishini humo umuhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuzidi kushikana.

“Nilikuwa nikikaa huko Uganda bila kuja maeneo haya yote. Lakini sasa nimekuja kama mtalii na haya ndiyo tunayofaa kuzidi kukuza. Wakenya na Waganda ni watu wamoja na tuzidi kushirikiana kwa faida zetu,” Besigye aliongeza.

Alitoa wito kwa viongozi wote wa Afrika kuunganisha bara hili kwa kujenga umoja na undugu baina ya watu.

Aliwataka marais Waafrika waliomo mamlakani kutokuwa viongozi wa kukandamiza raia, bali wa kuboresha viwango vya maisha yao kwa kuwapa huduma nzuri.

Mazishi hayo ya mwendazake Kegoro yalihudhuriwa pia na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga na aliyekuwa mwaniaji mwenza wake katika uchaguzi mkuu 2022, Martha Karua.

Bw Odinga aliibua ucheshi pale aliposema kwamba ikiwa kuna mtu anayefahamu jinsi mwaniaji huhisi wakati kura huibiwa, basi hakukuwa na mfano mwingine bora kuliko Bw Besigye.

Viongozi wengine kutoka jamii ya Abagusii pia walihudhuria hafla hiyo ya buriani.

Wote walimtaja mwenda zake kama kiongozi shupavu aliyewatumikia raia wake kwa bidii wakati wa uongozi wake.

 

  • Tags

You can share this post!

Raila aonya siasa isiingiziwe usimamizi wa Mumias

Wanawake wahalifu walivyomgeuza kiwete

T L