• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Chakula kibovu: Mpishi shuleni Mukumu afunguka

Chakula kibovu: Mpishi shuleni Mukumu afunguka

NA HELLEN SHIKANDA

WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu alitua katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Mukumu Aprili 15, 2023, na kumwondoa mwalimu mkuu pamoja na wanachama wa bodi ya wasimamizi akinuia kumaliza zimwi la magonjwa ya kiajabu shuleni humo.

Hata hivyo, wiki hii, mwezi mmoja baada ya shule hiyo kufunguliwa na wanafunzi kurejelea masomo, zimwi hilo limerejea na kuandama wanafunzi 82.

Limekatiza masomo ya wasichana hawa, kwa muda, ili watibiwe huku wadau wakiendelea kujikuna kichwa kuhusu asili ya ugonjwa huo.

Ikiwa vimelea vingeongea vingeungama kosa la kusababisha mahangaiko katika shule hii ya Upili ya Wasichana ya Mukumu inayoenziwa na watu wa Kakamega na maeneo mengine.

Mwezi mmoja uliopita, wanafunzi wa shule hii walilazwa katika hospitali mbalimbali walipodhihirisha dalili za kuhara, kutapika na kuumwa na tumbo.

Baada ya habari kuhusu madhila ya wanafunzi wa Shule ya Upili ya Mukumu kuonekana kutulia, waandishi wa Taifa Leo walielekea Magharibi mwa Kenya kujaribu kupata majibu ya maswali ambayo yamezonga vichwa vya wengi.

Shuleni humo, tulikutana na Douglas Muchela, mpishi ambaye amehudumu shuleni humu kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Douglas Muchela Isutsa ni mpishi shuleni Mukumu. PICHA | ISAAC WALE

Aliajiriwa katika shule hiyo ya Upili ya Wasichana ya Mukumu mnamo 2003, akaondoka baada ya kupata kazi nyingine kisha akarejea shuleni ambako sasa anatarajia kustaafu hivi karibuni.

Tulikutana na Bw Muchela siku moja baada yake kuondoka hospitalini baada ya kuonyesha dalili zilizofanana na zile za wanafunzi.

“Nimefanya kazi kama mpishi kwa muda mrefu na huwa nafahamu haraka ikiwa chakula kina kasoro. Nikibaini shida yoyote huwa ninasema haraka,” anasema.

Bw Muchela anachemka kwa hasira anaporejelea jikoni ambayo ilimfanya kukosana kila mara na mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Mukumu na wanachama wa bodi ya wasimamizi.

“Nyakati fulani huwa tunaletewa nyama mbovu ambayo haiwezi kuliwa. Nikibaini hilo, huwa nagoma na kusema sitaipika. Msimamizi wetu angeniripoti kwa Mwalimu Mkuu ambaye angeniita na kuniamuru nipike nyama hiyo,” akasema.

Bw Muchela anaongeza: “Hilo likifanyika, walimu hususia kula nyama hiyo lakini wanafunzi huwa hawana jingine ila kuila. Mara nyingi matokeo huwa mabaya.”

Mnamo Machi 15, 2023 kabla ya wanafunzi wengi kuugua baada ya kula chakula kibovu, Bw Muchela anaambia Taifa Leo kwamba alienda kwa afisi ya Mwalimu Mkuu, aliyefurushwa Aprili 16, kwa hiari yake, kutoa ripoti kuhusu hali ya chakula na jikoni.

“Nilimwambia kwamba jikoni ilikuwa katika hali mbaya. Ugali ulikuwa ukitoa harufu mbaya na haungeliwa. Mwalimu Mkuu alimuagiza mpishi mkuu na msimamizi na mpishi mmoja, wafike afisini mwake. Lakini wote hao, walisema mimi ni mchochezi na nilifaa kuhamishwa hadi idara nyingine,” Bw Muchela anasema.

  • Tags

You can share this post!

Wakili ataka TI Kenya itoe hoja nzito za kumpokonya Haji...

Koech, Were, Nusra na Mweresa watawala riadha za KDF siku...

T L