• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
COTU sasa yatisha kuitisha mgomo kupinga ushuru

COTU sasa yatisha kuitisha mgomo kupinga ushuru

NA CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) umetisha kuitisha mgomo ikiwa serikali itafeli kukinga wafanyakazi dhidi ya makali ya kupanda kwa bei ya mafuta na viwango vya juu vya ushuru.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, Naibu Katibu Mkuu wa muungano huo, Benson Okwaro, alisema ikiwa serikali haitawakinga wafanyakazi, COTU haitakuwa na jingine ila kuitisha mgomo wa kitaifa.

“Tunapinga vikali mtindo huu wa serikali kuongeza ushuru na kuanzisha makato mengine yanayoumiza zaidi wafanyakazi. Pamoja na hayo, tunaitaka serikali kubuni mbinu na njia za kupunguza bei ya mafuta. Ikiwa serikali haitachukua hatua za haraka kuwakinga wafanyakazi, tutalazimika kuwashauri wasusie kazi,” akasema Bw Okwaro.

“Wafanyakazi nchini ndio wanaumizwa zaidi na kupanda kwa gharama ya maisha kwa sababu mishahara yao ni duni japo serikali inazidi kuwaongezea mzigo mwingine wa ushuru,” akaongeza afisa huyo ambaye alikuwa ameandama na viongozi wengine wa COTU.

Aidha, COTU imetoa tishio hilo baada ya Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) kuongeza bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hili.

Bei ya mafuta aina ya petroli ilipanda kwa Sh16.6 kwa lita moja, ile ya dizeli ikaongezeka kwa Sh21.65 huku bei ya mafuta taa, yanayotumiwa na Wakenya wengi wenye mapato ya chini, ikipaa kwa Sh33.31.

Hii ina maana kuwa kuanzia Septemba 15, 2023 hadi Oktoba 15 mwaka huu, petroli itauzwa kwa Sh211.64 kwa lita jijini Nairobi.

Dizeli itauzwa kwa Sh200.62, huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh202.13.

Katika maeneo ya mashambani, bidhaa hizi zitauzwa kwa bei ya juu zaidi kuliko zinavyouzwa Nairobi na viunga vyake kutokana na gharama ya usafirishaji.

Hii ndiyo mara ya kwanza katika historia ya Kenya kwa bei ya bidhaa hizo za petroli kuuzwa kwa zaidi ya Sh200.

Kutokana na ongezeko hilo, Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) kilitangaza nyongeza ya nauli kwa kati ya asilimia 20 na asilimia 30.

Kulingana mwenyekiti wa muungano huo, Albert Karakacha, nauli itapanda kwa kima cha asilimia 20 katika barabara za maeneo ya miji na asilimia 30 kwa magari ya masafa marefu.

Aidha, inatarajiwa kuwa bei ya bidhaa za viwandani na mazao ya kutoka mashambani itapanda, hali ambayo itawalemea zaidi raia.

Licha ya bei ya mafuta kupanda kiasi hicho, Waziri wa Kawi, Davis Chirchir, aliwaambia wabunge, Ijumaa, kwamba serikali haina uwezo wa kudhibiti hali hiyo.

“Bei za mafuta zimepanda katika masoko ya kimataifa. Kwa hivyo, serikali haina uwezo wa kuzuia hali hiyo kwa sababu nchi huagiza mafuta kutoka ng’ambo,” Bw Chirchir akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Kawi, katika majengo ya bunge, Nairobi.

 

  • Tags

You can share this post!

Naibu gavana Kericho ampa gavana masharti kuhudumu naye

Ukatili: Mwanafunzi wa UoN akifumaniwa akimnajisi dadake  

T L