• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
DPP alegea kuwahoji mashahidi kwenye kesi dhidi ya Henry Rotich

DPP alegea kuwahoji mashahidi kwenye kesi dhidi ya Henry Rotich

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameonyesha kulegea kutoa ushahidi madhubuti katika kesi inayomkabili aliyekuwa waziri wa Fedha Henry Rotich ya ubadhirifu wa Sh63 bilioni katika kashfa ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Hii ni baada ya DPP kukataa kuwahoji mashahidi watano waliofika kortini.

Kutohojiwa kwa mashahidi hao na kiongozi wa mashtaka Geoffrey Obiri kumeanza kutoa nyufa za kusambaratika kwa kesi hiyo.

Mashahidi aliokataa kuwahoji Bw Obiri ni Boniface Mamboleo, Festus Kivisu, Maina Kiondo, Benedict Omondi na Kimani Kiiru

Mashahidi hawa ni maafisa kutoka wizara mbalimbali na Mamlaka ya Mazingira Nchini (NEMA).

Kutohojiwa kwa mashahidi hawa watano kumefikisha sita idadi ya mashahidi ambao Bw Obiri na wakili Oliver Mureithi wamekataa kuwauliza maswali.

Wiki iliyopita Bw Obiri alikataa kumhoji aliyekuwa Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya.

Mashahidi hao walikuwa wameagizwa wakamatwe Jumatatu walipokosa kufika kortini.

Walipofika kortini Jumanne wameomba msamaha.

“Niko na mashahidi watano waliofika kortini. Niko tayari kuendelea na kesi,” Bw Obiri alimweleza hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bi Eunice Nyuttu.

“Apisha mashahidi,” Bi Nyuttu alimwagiza karani wa mahakama.

Baada ya kuapishwa Bw Obiri alisema, “Sina maswali kwa hawa mashahidi.”

Aliposema hayo Bi Nyuttu aliwaruhusu mashahidi kuondoka mahakamani.

Pia Bw Obiri aliwasilisha barua kutoka kwa afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG) ikisema mashahidi wawili watafika kortini.

“Mashahidi wawili watafika kortini kesho Jumatano kutoka afisi ya CAG,” alisema Bw Obiri.

Hata hivyo, hakimu aliamuru kesi iendelee kesho Jumatano.

Na wakati huo huo, Bw Obiri aliwasilisha kesi ya kumtaka Bi Nyuttu ajiondoe katika kesi hiyo akidai “anaonea upande wa mashtaka na maafisa wanaochunguza kesi hiyo.”

Pia amesema Bi Nyuttu analazimisha upande wa mashtaka kuendelea na kesi ilhali mashahidi hawapo.

Bi Nyuttu aliwataka mawakili wa washtakiwa wajibu madai hayo.

Ombi hilo litasikilizwa Septemba 26, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Raila achamba serikali kwa kuuzia wakulima ‘mbolea ya...

Ojienda, Jalang’o wapata afueni ODM ikizimwa kuwatimua

T L