• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
El-Nino: Gachagua, magavana waendelea kupakana tope

El-Nino: Gachagua, magavana waendelea kupakana tope

NA WINNIE ATIENO

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameendelea kusuta magavana kutokana na janga la mafuriko nchini akisema kazi yao kubwa ni kufanya vikao na wanahabari kwa nia ya kulalamika.

Bw Gachagua alisema magavana wamekuwa wakishinda kwenye vyombo vya habari kueleza masuala ya mafuriko badala ya kwenda sehemu zilizoathirika kusaidia wahanga.

Akiongea huko Tana River, Bw Gachagua alisema ni sharti magavana waende mashinani ambapo Wakenya wameathirika na mafuriko badala ya kufanya vikao vya kulalamika tu.

Naibu Rais alisema ameshuhudia madhara ya mafuriko hasa katika kaunti za Garissa, Tana River na Mombasa hapo awali akieleza kuwa Rais William Ruto ameahidi kuwa hakuna Mkenya ambaye atakufa njaa kwa sababu ya mafuriko.

Alimpongeza Gavana wa Tana River, Dadho Godhana, kwa juhudi zake za kusaidia wakazi waliaothiriwa na mafuriko.

“Ndiyo maana tunataka tushikane kati ya Serikali Kuu na ile ya kaunti tusaidie waathiriwa. Tumefurahi kumpata Gavana papa hapa mashinani mahala wananchi wako. Wenzako wengine wameshinda kwenye vyombo vya habari wakipiga kelele. Hakuna lolote ambalo linaweza kutatuliwa kwenye vyombo vya habari,” akasema Bw Gachagua.

Hii ni baada ya Baraza la Magavana kufanya kikao na wanahabari wiki mbili zilizopita na kumshtumu Bw Gachagua kwa ‘kuhadaa’ Wakenya kuwa kaunti zimetumiwa fedha za kusaidia waathiriwa wa mafuriko.

“Shida za mafuriko ziko mashinani mahali wananchi wako, nendeni huko mjue shida iko wapi. Mahali dawa au chakula inatakikana unasaidia. Tusaidianeni katika hili janga la mafuriko,” alisema Bw Gachagua.

Alisema Serikali Kuu imejizatiti kutoa ndege, magari ya jeshi na helikopta kusaidia wahanga wa mafuriko. Alisisitiza kuwa serikali pia imesambaza dawa za matibabu, neti za mbu na vyakula ambavyo vinakusudiwa kusaidia waathiriwa.

“Tunahakikishia wananchi kuwa tunaelewa changamoto mnazopitia na si mwaka huu tu, hata miaka iliyopita kutokana na mafuriko ambayo yamekuwa yakiwahangaisha kila mwaka,” alisema Bw Gachagua.

Alimsihi Gavana Godhana kujiunga na chama tawala cha Kenya Kwanza ili anufaike zaidi na matunda ya serikali. Gavana Godhana alisema kaunti yake imeathirika pakubwa kwa sababu Tana River iko katika nyanda za chini.

“Kuna mito mingine midogo 10 ambayo imefurika kutokana na mvua na kumwaga maji yote katika Mto Tana. Asilimia 70 ya kaunti hii imeathiriwa na mafuriko na hiyo ni idadi ya takriban watu 200,000 ambao hawawezi kupata huduma muhimu,” alisema Bw Godhana.

Gavana huyo alisema ametumia raslimali zote za kaunti kusaidia wahanga wa janga la mafuriko baada ya nyumba zao kufurika na mali kusombwa na mafuriko.

“Tumekata miradi yote ili kuleta pesa kusaidia watu lakini mambo bado ni magumu zaidi,” alisema Bw Godhana.

Haya yanajiri huku Mwakilishi wa wadi wa eneo la Garsen Kusini Bw Sammy Dumbe kuomba msaada akisema vijiji vya Wema, Hewani, Kulesa, Vumbwe, Lazima, Mwangaza, Peponi na Mikameni ambavyo vina idadi ya zaidi ya watu 20,000 huku wakihitaji chakula, matibabu na maji ya kunywa.

  • Tags

You can share this post!

Safaricom yamwagia East African Safari Classic Rally...

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama atishiwa...

T L