• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Gachagua adai Uhuru Kenyatta alifumbia macho pombe haramu na dawa za kulevya

Gachagua adai Uhuru Kenyatta alifumbia macho pombe haramu na dawa za kulevya

Na WANGU KANURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amelaumu serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kutopigana sawa sawa na biashara ya pombe haramu na dawa za kulevya nchini.

Akizungumza kwenye kikao na washikadau jinsi ya kumaliza pombe haramu na dawa za kulevya katika Bonde la Ufa, Bw Gachagua alisema kuwa wengi humkashifu kwa kulaumu serikali iliyokuwepo lakini yeye husema ukweli.

“Hali hii ilidorora kabisa wakati wa serikali hiyo nyingine. Hawakujali hata. Watu waliuza pombe saa zisizostahili, wengine pombe haramu huku maafisa wakitazama tu. Lakini sitawalaumu maafisa. Hawakuongozwa inavyofaa,” akaeleza.

Hata hivyo, Bw Gachagua alisema kuwa wakati Rais William Ruto alichukua usukani, alitatizika sana na jinsi maafisa wote wa serikali kuu walitekeleza wajibu wao.

“Wengi walikuwa wameacha kazi zao na kujiunga na siasa. Rais Ruto alishangaa sana kwa nini ilhali kitengo cha polisi ni kikuu katika uendeshaji wa nchi,” akasema.

Baada ya mazungumzo ya kina na Rais Ruto, Bw Gachagua alimhakikishia kuwa maafisa hao walikuwa wazuri ni vile serikali iliyokuwa inawaongoza haikuwaonyesha njia.

“Kazi ya maafisa ni kuhakikisha kuwa kuna usalama, hakuna wizi wa mifugo, wauzaji na wapikaji pombe haramu wamekamatwa lakini wale waliokuwa serikalini walikuwa wamepewa majukumu ya kuokota saini za kuunga mkono BBI pamoja na kuuza sera za Azimio.”

BBI ni mswada maarufu uliolenga kufanya mabadiliko ya Katiba, japo uliangushwa na Mahakama ya Juu zaidi nchini ikiutaja kama haramu na ambao sheria hazikufuatwa kuuanzishwa.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua – Nilikuwa mlevi kabla kuokoka

Vijana wa kurandaranda mtaani watupa mwili katika lango la...

T L