• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Hatimaye Serikali yatoa Sh10 bilioni kukabili athari za El Nino

Hatimaye Serikali yatoa Sh10 bilioni kukabili athari za El Nino

BENSON MATHEKA Na FRIDAH OKACHI

HATIMAYE serikali ya Kitaifa imetoa Sh10 billioni kwa serikali za Kaunti ili kukabiliana na athari za mvua ya El-Nino inayoendelea kunyesha nchini.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri (CoG) uliofanyika Jumatatu, Novemba 27, 2023 uliidhinisha Wizara ya Fedha kutoa pesa hizo kusaidia watu waliopoteza makao, kufurushwa makazini na kukumbwa na hatari ya milipuko ya magonjwa, kurekebisha uharibifu wa miundomsingi na mali.

Taarifa kutoka Ikulu ilisema kaunti 38 kati ya 47 zinakumbwa na mafuriko ambayo yameangamiza watu 76 huku familia 35,000 zikihama makazi yao hasa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki, Mashariki na Pwani.

Serikali pia, kupitia Hazina Kuu imetenga Sh500 milioni kusaidia kampuni za maziwa nchini kununua maziwa ya ziada katika msimu huu wa mvua.

Pia Sh180 milioni zitatumiwa kununua vifaa vya matibabu.

Juma lililopita, Naibu wa Rais Bw Gachagua kwenye ziara yake Mombasa alisema magavana walikuwa wamepokea pesa za kukabiliana na El Nino.

“Hatutaki kuona gavana yeyote akilaumu serikali ya kitaifa kwa kukosa kusambaza chakula. Kama serikali tulitoa Sh10 bilioni kwa shughuli hii,” alisema awali akiwa Mombasa.

Baadaye akiwa Nairobi alisema: “Tunashangaa kuona magavana wakilalamika kwamba hawajapokea pesa za El Nino kutoka kwa serikali ya kitaifa. Hakuna pesa kama hizo watapata. Wanapaswa kutumia pesa za dharura wanazotenga katika bajeti za mwaka kusaidia watu wanaotawala.”

Magavana wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza lao (CoG), Anne Waiguru, walimfunza Bw Gachagua mambo anayopaswa kujua vyema kwa kumjulisha kuwa pesa za El Nino hazikutumwa kwa kaunti na hawajapokea mgao wowote kutoka kwa serikali ya kitaifa wa kima cha Sh62 bilioni.

“Kufikia sasa, tunataka kusema serikali za kaunti, hazijapokea mgao wowote kutoka kwa serikali ya kitaifa kutekeleza hatua za kukabiliana na El Nino. Kaunti zinadai mgao wa jumla ya Sh62.3 bilioni ambazo bado hazijatolewa. Tunachukulia matamshi hayo (ya Gachagua) kuwa dhidi ya moyo wa ushirikiano wa viwango viwili vya serikali inavyohitaji ibara ya 6(2) ya Katiba,” akaeleza Bi Waiguru kwa niaba ya magavana wote 47.

 

  • Tags

You can share this post!

KNEC yatakiwa kuangazia dosari za KCPE kama kura za urais...

El Nino: Hofu nyanda za juu Pokot Magharibi mmomonyoko wa...

T L