• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Hatimaye Wapokomo wapata toleo la Biblia kwa lugha yao

Hatimaye Wapokomo wapata toleo la Biblia kwa lugha yao

NA ALEX KALAMA

WAUMINI wa dini ya Kikristo kutoka jamii ya Wapokomo ambao wengi wao ni wenyeji wa Kaunti ya Tana River, sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kupata Biblia iliyoandikwa kwa lugha yao.

Kasisi Peter Munguti amewataka waumini wa dini ya Kikristo kutoka jamii ya Wapokomo kusoma Biblia hiyo vyema na kuielewa ili kujiepusha na kupotoshwa na mafunzo potovu.

“Katika siku za hapo nyuma baadhi ya watu wamekuwa wakipotoshwa kiimani na wahubiri ambao wamekuwa wakifasiri Biblia vibaya kutokana na kwamba Biblia mara nyingi katika maeneo haya huwa imeandikwa kwa lugha mbili pekee – Kiingereza na Kiswahili. Lakini sasa nafikiri jambo hilo mtaweza kuliepuka kwa sababu Biblia hii imeandikwa kwa lugha yenu ili muweze kuelewa kwa urahisi,” alisema Bw Munguti.

Kasisi huyo alisema kuwa zaidi ya miaka 38 waumini wa dini ya Kikristo kutoka jamii ya Wapokomo walikuwa na ndoto ya kupata Biblia iliyoandikwa kwa lugha yao.

Boksi lenye nakala za Biblia toleo la lugha ya Kipokomo likifunguliwa kijijini Isdowe, eneobunge la Garsen, Kaunti ya Tana River. PICHA | ALEX KALAMA

Hatimaye ndoto hiyo imeweza kutimia baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Biblia hiyo mnamo Jumamosi.

“Haikuwa kazi rahisi kwa sababu safari hii imechukua miaka 38 hadi kupata toleo la Biblia iliyoandikwa kwa lugha ya Kipokomo. Mnaweza kuitumia katika kuwafundisha watoto wenu jinsi ya kukua kiimani na kuenenda kwa njia inayompendeza Mwenyezi Mungu,” alisema Kasisi.

Kwa upande wake, Seneta wa Tana River Danson Mungatana aliwahimiza Wapokomo kuitumia Biblia hiyo katika kuwaelekeza wana wao jinsi ya kuwa na maadili mema.

“Mimi langu ni kuwasisitizia tu kwamba kupata toleo la Biblia kwa lugha ya Kipokomo ni ufanisi hivyo muitumieni vyema. Kila mmoja miongoni mwetu asiyejua Kiswahili na Kiingereza vizuri atasoma na kuelewa kilichoandikwa kwa toleo la Kipokomo,” alisema Bw Mungatana.

Jumla ya nakala 4,000 za Biblia toleo la lugha ya Kipokomo zilizinduliwa mnamo Jumamosi katika kijiji cha Idsowe eneobunge la Garsen kwenye ukumbi wa kanisa la African Inland Church of Kenya (AIC).

Kwenye hafla iliyohudhuriwa na viongozi mashuhuri akiwemo Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi, Gavana wa Tana River Gadho Godana, Seneta wa Tana River Danson Mungatana na seneta maalum Rapheal Chimera.

  • Tags

You can share this post!

UDA yaanza kuiga makosa ya Jubilee

Fahamu chimbuko la Kiunga, mji wa Lamu Mashariki wenye...

T L