• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola sasa yagonga 251

Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola sasa yagonga 251

ALEX KALAMA Na FARHIYA HUSSEIN

MAAFISA wanaoendelea na shughuli ya ufukuaji wa makaburi katika msitu wa Shakahola wamepata miili tisa katika siku ya kwanza ya awamu ya tatu ya ufukuaji huo ambao umezinduliwa rasmi Jumanne na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki.

Akizungumza na wanahabari Mshirikishi wa ukanda wa Pwani Rhoda Onyancha amedokeza kuwa hadi kufikia sasa jumla watu 251 wamethibitishwa kufariki huku idadi ya waliookolewa ikifika watu 95.

“Leo tumefukua miili tisa huku wale ambao tumewakamata kuhusiana na mauaji hayo wakiwa ni watu 35,” alisema Bi Onyancha.

Hadi kufikia sasa watu 19 wameunganishwa na familia zao huku familia 613 zikisalia bila ufahamu wa walipo wapendwa wao.

Haya yanajiri huku siku sita zikipita bila uokozi wa mtu yeyote ndani ya msitu wa Chakama.

Aidha Waziri wa Usalama Kithure Kindiki amedokeza kuwa serikali kwa ushirikiano na wanajeshi na masoroveya wanajenga barabara ndani ya chaka la mauti la Shakahola ili kuwawezesha maafisa kuingia ndani zaidi na kuendelea na operesheni.

“Tunatengeneza njia nyingi zaidi ili kurahisisha harakati za uokoaji wa wale manusura waliosalia ndani ya msitu. Kufanya hivyo pia kutatusaidia kuimarisha operesheni hii,” akasema Bw Kindiki.

Aidha waziri Kindiki amesisitiza kuwa serikali imekusanya ushahidi wa kutosha kuhakikisha kuwa mshukiwa mkuu Paul Mackenzie na wenzake wanapewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Waziri amedokeza washukiwa hao wanaweza kushtakiwa kwa kutekeleza kosa la mauaji ya halaiki.

  • Tags

You can share this post!

Taharuki magenge ya uhalifu yakihangaisha watu Nakuru

Sakata ya Kemsa: Terry Ramadhani adai waziri Nakhumicha...

T L