• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
IPOA yaanzisha uchunguzi baada ya polisi kuua raia sita Isebania

IPOA yaanzisha uchunguzi baada ya polisi kuua raia sita Isebania

NA WYCLIFFE NYABERI

MAMLAKA Huru ya Kuangalia Utendakazi wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo polisi waliwapiga risasi na kuwaua watu sita katika Kaunti ya Migori.

Inadaiwa sita hao walikuwa miongoni mwa watu waliovamia kituo cha polisi cha Isebania mnamo Alhamisi wakiwa wamejihami kwa mapanga na mawe.

Raia hao wenye hasira kulingana na polisi, walikuwa kwenye msafara uliokuwa umetoa mwili wa mkazi mmoja kutoka kwenye hifadhi moja ya maiti.

Lakini walipofika kituoni, walikivamia wakitaka majibu ni kwa nini kumekuwa na visa vya utovu wa usalama katika sehemu hizo.

Walianza kuyavunja madirisha na milango ya kituo hicho huku wakiwa na lengo la kuiba bunduki na kuwafungulia waliokuwa kwenye seli kulingana na ripoti ya polisi.

Kwa kuona wamezidiwa nguvu na ghala la silaha limevamiwa, polisi hao walifyatua risasi kujaribu kuwatawanya lakini wakadai kwa bahati mbaya risasi hizo zilileta maafa.

Katika taarifa, IPOA imesema ilifahamu kisa cha ufyatuaji risasi katika kituo cha polisi cha Isebania katika Kaunti Ndogo ya Kuria Magharibi, ambapo watu sita waliripotiwa kuaga dunia na wengine wakajeruhiwa vibaya.

“Ofisi yetu ya Kanda ya Kisumu katika hoja yake Ijumaa asubuhi ilituma kikosi cha kudadarukia masuala ibuka kuanzisha uchunguzi kuhusu vifo na majeruhi. IPOA pia inatoa wito kwa umma kudumisha amani na kufuata sheria wakati mamlaka inapochunguza suala hilo,” inasema sehemu ya taarifa ya mamlaka hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti Anne Makori.

Ripoti ya awali ya polisi wa Migori ilionyesha kuwa mmoja wao aliyekuwa akisimamia pahala silaha zao huhifadhiwa alijeruhiwa jicho katika vurumai hizo.

Walioangamia walipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya St Akidiva Mindira Mabera.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Machogu kuzindua rasmi kituo cha maji safi shuleni...

Hellen Obiri alenga kutetemesha kwenye New York City...

T L