• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Jamaa wa wanaume sita walioshtakiwa kwa wizi wa Sh94 milioni walia mahakamani

Jamaa wa wanaume sita walioshtakiwa kwa wizi wa Sh94 milioni walia mahakamani

NA RICHARD MUNGUTI

JAMAA wa wanaume walioshtakiwa kwa wizi wa Sh94 milioni za dukakuu la QuickMart wamelia mahakamani baada ya sita hao kuachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni kila mmoja.

“Sasa tutatoa wapi Sh4 milioni? Watu wetu watapata taabu,” mamake mmoja wa washtakiwa hao amesikitika.

Jamaa hao walikaa sakafuni huku wakilia kwa vikundi.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Lucas Onyina aliwaachilia washtakiwa hao kwa dhamana ya Sh4 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho kila mmoja.

Katika uamuzi wake, Bw Onyina alisema kiwango cha pesa zilizoibwa ni kikubwa mno na polisi wanaendelea kuandama washukiwa wengine.

Ijumaa wiki iliyopita, Bw Onyina aliamuru washtakiwa wazuiliwe gerezani ajifahamishe na ripoti ya urekebishaji tabia ya washtakiwa.

“Nahitaji muda kusoma na kujifahamisha na ripoti za urekebishaji tabia za washukiwa wote sita ndipo niweke viwango vya dhamana,” Bw Onyina aliwaeleza washtakiwa Ijumaa.

Waliofikishwa kortini kuhusiana na wizi wa pesa hizo za QuickMart ni James Mbatia Kariuki, Ismael Patrick Gitonga, Martin Nderi Ng’ang’a, Joel Oyuchi Mwelesi, Harrison Mugendi Njeru na Ronald Ouma Oluu.

Sita hawa wanakabiliwa na shtaka la kula njama za kuiba Sh94,918,750 za QuickMart zilizokuwa zinapelekwa katika benki ya Family Bank mnamo Novemba 6, 2023.

Washukiwa hao pia wamefunguliwa shtaka la kupatikana na zaidi ya Sh9 milioni kati ya pesa zilizoibwa.

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa hao pamoja na washtakiwa wengine ambao hawakufikishwa kortini, waliiba Sh94,918,750 kutoka kwa gari la kampuni ya Wells Fargo nambari KBA 517 T lililokuwa linapeleka pesa hizo katika benki ya Family Bank.

Nderi Ng’ang’a alishtakiwa kupatikana Sh9,101,300 katika eneo la Roybain Heights kaunti ya Nairobi akijua zimeibwa ama kupatikana kwa njia isiyo halali.

Patrick Gitonga na Nderi Ng’ang’a wameshtakiwa kujaribu kupindua rangi ya gari nambari KBM 751W aina ya Toyota Fielder wakijua lilikuwa likitakiwa na polisi kwa tuhuma za kubeba pesa hizo zilizoibwa.

Washtakiwa walipatikana wakipaka gari hilo rangi mnamo Novemba 11, 2023, katika eneo la Mihang’o jijini Nairobi.

Ismael Mbatia na Patrick Gitonga walishtakiwa kwa kupatikana na sanduku lililokuwa linabebea pesa hizo.

Hakimu aliamuru idara ya magereza impeleke Gitonga hospitalini baada ya kudai alitandikwa na polisi na kupata majeraha.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yaipiga breki serikali kuuza KICC, mashirika...

Meneja afafanua ndege ilipata panchari ikitua uwanjani Manda

T L