• Nairobi
  • Last Updated May 30th, 2023 9:48 AM
Jamii ‘kutakasa’ mnara wa Ngala

Jamii ‘kutakasa’ mnara wa Ngala

Na MAUREEN ONGALA

JAMII ya Wamijikenda, inapanga kufanya matambiko ya kitamaduni katika sanamu ya marehemu Ronald Gideon Ngala, ambayo ilizinduliwa Nairobi na Rais Uhuru Kenyatta wiki iliyopita.

Bw Noah Katana Ngala, ambaye ni mwanawe marehemu, alisema familia haina pingamizi kwa mpango huo wa jamii ya Wamijikenda.

“Kama jamii inaonelea inahitaji kufanya chochote kumsherehekea Ngala basi sisi hatuwezi kuingilia na kuwakataza. Ngala alikuwa ni wa Kilifi, nyumbani kwake na vile vile Kenya nzima kwa vile alikuwa kiongozi wa kitaifa,” akasema.

Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire, alifichua kuwa mashauriano yanaendelezwa baina ya jamii za Wamijikenda na jamii nyingine za Pwani pamoja na viongozi wa Chama cha KADU ili kupanga jinsi sherehe hiyo inavyoweza kufanikishwa.

Kulingana naye, miongoni mwa mambo ambayo yanawaziwa katika matambiko hayo ya kitamaduni, ni nyimbo na densi za Kimijikenda, kunywa na kutema pombe ya mnazi, miongoni mwa mambo mengine.

“Mnara huo umedhihirisha kuwa jamii ya Wamijikenda inatambuliwa kikamilifu. Mzee Ngala alipigania majimbo. Kwa miaka mingi tulizunguka kama nchi lakini mwishowe tukachagua ugatuzi ambao si tofauti na utawala wa majimbo,” akasema.

Mnara huo ulijengwa kupitia kwa Wizara ya Michezo, Utamaduni na Turathi inayosimamiwa na Bi Amina Mohamed.

Bw Katana Ngala, ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo, alisema hatua ya Rais Kenyatta kuzindua mnara huo Nairobi, ilipokewa kwa heshima kubwa na familia yake pamoja na jamii za Kilifi kwa ujumla, kwani ni jambo ambalo wamelisubiri kwa miaka mingi.

“Kutokana na kuwa yeye ni Mmijikenda, ni furaha kuu kwa Wamijikenda kuwakilishwa kupitia kwa mnara huo. Sote tunajua mchango ambao Ngala aliutoa kuhakikisha nchi hii inapata uhuru kupitia kwa Majimbo ambayo ilipelekea kuundwa kwa mikoa minane,” akasema.

Mbunge huyo wa zamani wa Ganze ambaye aliwahi kutumikia baraza, alitoa changamoto kwa jamii za Pwani kuungana na kutumia vyema ugatuzi kuboresha maisha na maendeleo.

“Kila mara huwa tunatoa wito kwa umoja wa Pwani kisiasa na kimaendeleo. Viongozi wanafaa waungane ili kuhakikisha ugatuzi utatuletea maendeleo ambayo yatasaidia watu wetu,” akasema.

Alieleza kuwa, familia yake itaendelea kupigania maono ya marehemu kupitia kwa chama cha Kadu Asili ambacho kinaendelea kupanga mikakati yake kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu ujao.

Mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana, alitoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi kujenga makavazi maalumu katika boma la marehemu ili vizazi vya sasa na vijavyo, viendelee kukumbuka mchango wake kwa siasa na maendeleo ya Pwani na taifa zima kwa jumla.

Mbunge huyo alieleza wasiwasi kuwa, huenda historia yake ikasahaulika katika kaunti iwapo hakuna hatua zitachukuliwa kuhifadhi kumbukumbu zake ipasavyo.

Vile vile, alitoa wito kwa serikali kutia lami kwa barabara ya kilomita tatu kutoka Bondora hadi Mwakombe kwa heshima za marehemu.

You can share this post!

ODM yamkubali Kingi kwa masharti

TAHARIRI: Mafuriko: Mikakati ya kuzuia hasara ibuniwe

T L