• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Kaunti za Pwani zatakiwa kufunza vijana kuthamini wazee kukomesha mauaji ya wakongwe

Kaunti za Pwani zatakiwa kufunza vijana kuthamini wazee kukomesha mauaji ya wakongwe

NA ALEX KALAMA

WITO umetolewa kwa serikali za kaunti sita za Pwani pamoja na serikali kuu kushirikiana na kutenga fedha za kuendesha hamasisho la kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wa wazee katika jamii.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, mwanaharakati Caroline Ngorobi kutoka kikundi cha Jukwaa Arts alisema vijana katika ukanda wa Pwani hususan wa jamii ya Mijikenda hawana ufahamu kuhusu maswala ya mila na tamaduni zao, hali ambayo imewafanya wengi wao kuwadharau wazee.

“Vijana wengi hawajui umuhimu wa mila na utamaduni na ndiyo maana wakiambiwa huyu ni mzee wa Kaya wao husema ni mchawi. Lakini wakifundishwa na kuelewa vizuri kazi ya mzee wa Kaya ni nini basi visa vya wazee kuuawa kwa kisingizio cha uchawi vitaisha,” alisema Bi Ngorobi.

Mwanaharakati Caroline Ngorobi kutoka kikundi cha Jukwaa Arts akitabasamu. PICHA | ALEX KALAMA

Kulingana na Bi Ngorobi ni kwamba kuna haja ya serikali zote mbili kulichukulia kwa uzito jambo hilo na kulifanyia kazi ili kuhakikisha wazee wote wanalindwa ili kuhifadhi historia kwa vizazi vijavyo.

“Wajua hakuna kitabu ambacho kimeandikwa na kuhifadhiwa ambacho kinaelezea historia ya jamii ya Wamijikenda isipokuwa ukitaka kujua vizuri kuhusu jamii utaambiwa nenda kwa wazee wa Kaya watakueleza. Kwa hivyo kuna umuhimu wa hawa wazee kutunzwa. Na pia kuna umuhimu wa vijana kuelimishwa ili wajue umuhimu wa mila na utamaduni,” alisema Bi Ngorobi.

Hata hivyo, Bi Ngorobi alidokeza kuwa kikundi hicho kimejitolea kuelimisha jamii hasa vijana kupitia sanaa ya uigizaji filamu kupitia programu wanayoiita Chimidzimidzi ambayo wanaifanya katika kaunti tatu za Pwani – Mombasa, Kwale na Kilifi.

Programu hiyo ilipata ufadhili kutoka kwa Ignate Culture kwa ushirikiano na British Council of Kenya.

Kwa upande wake John Mumba ambaye ni mkuu wa uzalishaji filamu katika kikundi hicho, alisema kuna haja ya mila na tamaduni za jamii ya Wamijikenda pamoja na historia ya jamii hiyo kuandikwa na kisha turathi zake zihifadhiwe vizuri kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

“Tumeona jamii ya Wamaasai ikienzi na kuthamini utamaduni wao hapa nchini na bila shaka wamejituma na kuhakikisha wanatambulika karibu ulimwengu mzima kupitia huo utamaduni wao ambapo hadi sasa wananufaika na wanajiingizia kipato. Kwa hivyo hata sisi Wamijikenda hatuna budi kuiga mfano huo. Tuko na uwezo wa kunufaika kupitia utamaduni wetu,” alisema Bw Mumba.

  • Tags

You can share this post!

Mke hula kupita kiasi, nashindwa kumwambia

Mwanamuziki Muigai wa Njoroge akana ‘kumdhuru’...

T L