• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
KEBS: Mafuta yaliyosemekana kuwa hatari ni salama

KEBS: Mafuta yaliyosemekana kuwa hatari ni salama

NA CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) limefafanua mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini na Shirika la Kitaifa la Biashara (KNTC) ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Kupitia taarifa Jumatano, Desemba 6, 2023 Kebs ilisema kuwa mafuta hayo ya maji maji (salad) yaliyonunuliwa kutoka ng’ambo, yamefanyiwa ukaguzi hitajika na kubainika kuafiki viwango hitajika.

Hata hivyo, shirika hilo lilisema kuwa sampuli za mafuta hayo zilizochunguzwa hazikutimiza viwango hitajika vya madini ya Vitamin A.

“Kutokana na vipimo vilivyofanyika mafuta hayo yalifikia mahitaji yote ya kiafya na kiusalama yanayotumika nchini. Hata hivyo, sampuli zilizochunguzwa hazikuwa na viwango vinavyokubalika nchini vya Vitamin A. Hii sio kigezo cha kiafya na kiusalama na KEBS imewasilisha matokeo hayo kwa KNTC,” Kebs ikaeleza katika taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Taarifa hiyo kutoka Kebs inajiri kufuatia ripoti zilizotolewa hivi majuzi kwamba baadhi ya mitungi ya mafuta hayo ya kupikia yaliyochunguzwa hayakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Mafuta hayo yalikuwa yameagizwa kutoka ng’ambo mapema mwaka huu kama sehemu ya mkakati wa serikali kupunguza gharama ya maisha.

“Tunataka kuwahakikishia wananchi kwamba Kebs imejitolea kuhakikisha ubora za bidhaa zinazotengenezwa nchini na zile zinazoagizwa kutoka nje,” Kebs ikaeleza.

Wiki hii, maafisa wa KNTC walihojiwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutokana na tuhuma kwamba sheria haikufuatwa wakati wa utoaji wa zabuni ya uagizaji wa mafuta hayo ya kupikia ya thamani ya Sh9 bilioni.

00

  • Tags

You can share this post!

Ndovu wakaidi Taita Taveta ‘wanaonyang’anya’ watu...

LSK yawinda mawakili 21 bandia

T L