• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 7:00 AM
Khalwale ahimiza Ruto kufuta mawaziri wanaompotosha

Khalwale ahimiza Ruto kufuta mawaziri wanaompotosha

CECIL ODONGO na SHABAN MAKOKHA

MIITO kuwa Rais William Ruto atatekeleza mabadiliko kwenye Barazalake la Mawaziri imeanza kuibuka ndani ya Kenya Kwanza, huku kuwa taifa likielekea pabaya kiuchumi hasa baada ya kupanda kwa bei ya mafuta

Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale ametaka Ruto awafute kazi baadhi ya mawaziri aliodai wanamshauri vibaya kuhusu hali ya uchumi wa nchi.

Naye Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwenye taarifa, jana alidokeza kuwa huenda mabadiliko katika baraza la mawaziri yakafanywa “hivi karibuni” ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wakenya.

Hata ingawa hakutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo, alisema kuwa wote waliochaguliwa na Rais wanastahili kuwajibikia majukumu yao ipasavyo ili kuimarisha maisha ya Wakenya.

“Wakati ambapo afisa yeyote aliyechaguliwa na serikali anakiuka maadili ya kazi yake, Rais ana mamlaka ya kuchukua hatua kwa kutumia hekima yake na wakati ambao anataka kufanya hivyo,” akasema Bw Mudavadi.

Wakenya wamekuwa wakilalamika kuwa baadhi ya mawaziri katika utawala wa sasa wana utendakazi duni na hawaelewi majukumu yao.

Rais mwenyewe amewahi kukiri hadharani kuwa anafahamu baadhi ya masuala ndani ya wizara mbalimbali, kuliko hata baadhi ya mawaziri wanaohudumu kwenye nyadhifa hizo.

Bw Khalwale alimtaka Rais amtimue Waziri wa Biashara Moses Kuria, mwenzake wa Kawi Davis Chirchir na washauri wake kuhusu masuala ya uchumi, wakiongozwa na Dkt David Ndii.

Alisema maafisa hao ndio wa kulaumiwa kutokana na hali ngumu ya sasa ya kiuchumi ambayo inawaumiza raia.

“Ningetaka kukuambia Rais kuwa watu ambao umewateua ndio wamekufeli na lazima uwatimue mara moja. Wafute mawaziri wanaosimamia kawi na biashara pamoja na washauri wako kuhusu masuala ya kiuchumi kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta,” akasema Bw Khalwale.

Alikuwa akizungumza wakati wa mazishi ya Adriano Mukaisi katika eneobunge la Shinyalu mnamo Jumamosi, Septemba 16, 2023.

Marehemu ni babake Herbart Sore ambaye alikuwa msaidizi wa kibinafsi wa aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

Seneta huyo alizua maswali kwa nini sheria zinazodhibiti uagizaji wa bidhaa kutoka nje, 2023 zilikuwa zimekosa kutoa suluhu kwa bei ya petroli inayoendelea kupanda kila mara.

Bw Kuria alinukuliwa akiwataka Wakenya wajiandae kwa nyakati ngumu zaidi kwa sababu bei ya petroli itakuwa ikipanda kwa Sh10 kila mwezi hadi miezi mitano ikamilike.

“Nawajali wahudumu wa bodaboda na maskini ambao hawawezi kumudu bei ya petroli. Mambo yanaendelea kuwa mabaya na Rais anastahili kuwatimua mawaziri hao na washauri wake wa kiuchumi,” akasema Bw Khalwale.

Naibu Rais Rigathi Gachagua naye aliwachemkia mawaziri ambao wanazungumzia Wakenya kwa lugha mbaya, akisema wanastahili wafahamu wao ni watumishi wa umma na Wakenya ndio waliwaajiri.

“Humzungumzii mwaajiri wako ukiwa na kiburi bali lazima unyenyekee. Wakenya kama tu raia wa nchi nyingine wanapitia hali ngumu kiuchumi na kama viongozi tunastahili kuwajali. Viongozi wazuri huwapa matumaini waliowachagua,” akasema Bw Gachagua.

 

  • Tags

You can share this post!

Wavuvi wauana kwa sababu ya sigara ya Sh15

Kuria amjibu Gachagua akijigamba yeye ndiye ‘truthful...

T L