• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:30 PM
KNUT yasema haiwezi kumtetea mwalimu wa kuwataka watoto wa shule kimapenzi

KNUT yasema haiwezi kumtetea mwalimu wa kuwataka watoto wa shule kimapenzi

Katibu Mkuu wa chama hicho Collins Oyuu amesema Jumamosi kwamba ni kinyume cha maadili, na kanuni za taaluma ya ualimu, kwa walimu kushiriki uovu kama huo.

Akiongea mjini Kerugoya wakati wa Mkutano wa kila Mwaka wa KNUT, tawi la Kirinyaga, Bw Oyuu aliwataka walimu wa kiume kutoa nafasi kwa wanafunzi wa kike kuendelea na masomo bila kuwasumbua na kuwataka kimapenzi.

“Walimu wa kiume hawapaswi kuwatongoza wanafunzi wa kike kwa ajili ya kuwanyanyasa kingono. Wanafaa kuwaendea watu wazima kuliko kuwaharibu watoto wetu. Huu ni uovu ambao KNUT hatutauvumilia,” akasema kwa ukali.

Bw Uyuu aliamuru maafisa wa matawi yote ya chama cha KNUT kote nchini kuhakikisha kuwa “walimu hawajamiiani na wanafunzi wao”.

“Hatutawatetea au kuunga mkono walimu watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na shughuli za utovu wa maadili shuleni; walimu hawafai kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wao,” akasisitiza huku akishangiliwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo.

“Kama Katibu Mkuu sitakiwa kusikia chochote kuhusiana na madai ya walimu, wa jinsia zote mbili, kushiriki mapenzi na wanafunzi wao. Walimu ni baba na mama na hawafai kuwaharibu watoto wetu bali kuwafundisha na kuwaelekeza kimaadli,” Bw Oyuu akasisitiza.

Alilamikia kile alichokitaja kama kukithiri kwa visa vya walimu hata kuwabaka wasichana wasio na ufahamu na kuwachafua, akisema tabia kama hiyo inafaa kukoma.

“Wanafunzi wa kike sio wake au wapenzi, ni wanafunzi na sharti walindwe,” Bw Oyuu akaeleza huku akiongeza kuwa ni aibu kwa walimu kusimamishwa kazi kwa kuwanyanyasa kimapenzi wanafunzi wao.

Mwaka 2022, Tume ya Huduma za Walimu (TSC) iliwasimamisha kazi jumla ya walimu 41 makosa mbalimbali ikiwemo kushiriki mapenzi na wanafunzi wao.

Wakati huo huo, Bw Oyuu ameikosoa Baraza la Kitaifa la Walimu (KNEC) kwa kujivuta kuwalipa walimu waliosimamia mitihani ya kitaifa mwaka 2022.

Alisema kuwa walimu kama hao wanapasa kulipa marupurupu yao haraka baada ya wao kukamilisha zoezi hilo.

Bw Oyuu alisema KNUT inafuatilia suala hilo kwa karibu zaidi na haitaruhusu KNEC kuendelea kuchelewesha malipo ya walimu wanaosimamia mitihani ya kitaifa na kuisahihisha.

Afisa huyo alisema walimu hutia bidi kuhakikisha kuwa watahimiwa wanasimamiwa vizuri na karatasi za mitihani inasahihishwa na “hivyo wanafaa kuthaminiwa na kuheshimiwa kwa kazi hiyo kubwa”.

“Hatutaketi na kutazama huku walimu wetu wakiendelea kuteseka. Wanafaa kupewa haki yao baada ya mitihani ya KCPE na KCSE kukamilika na kusahihishwa,” Bw Oyuu akasema.

Katibu wa KNUT, tawi la Kirinyaga Bw Mwangi Kanaiyu aliunga mkono kauli hiyo na kukariri kuwa chama hicho kitaendelea kupigania masilahi ya walimu.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Power yawarai wawekezaji wa kibinafsi kuisaidia...

Arsenal moto balaa, Manchester machozi!

T L