• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 5:50 AM
Kondakta walia kulemewa kufikisha malipo ya siku kwa waajiri wao

Kondakta walia kulemewa kufikisha malipo ya siku kwa waajiri wao

NA RICHARD MAOSI

ONGEZEKO la bei ya mafuta petroli nchini imechochea magari ya uchukuzi na pikipiki katika sehemu nyingi za nchi kuongeza nauli mara dufu.

Wahudumu hao wa usafiri na uchukuzi, wameongeza ada kwa kati ya asilimia 20 hadi 50, hii ikiashiria Wakenya wanapaswa kujiandaa kwa hali ngumu ya maisha siku zijazo.

Aidha mzozo unatokota baina ya wamiliki wa magari na wafanyikazi wao, ikibainika itakuwa vigumu kufikisha kiwango cha pesa kinachohitajika kila siku almaarufu target, bila kusahau magari mengi ni ya mikopo.

Ingawa wamiliki wa matatu wiki iliyopita waliitisha kikao na wanahabari, walikubaliana kuwa nauli zitapanda kwa asilimia 20 pekee, lakini baadhi ya matatu zimepandisha zaidi ya maradufu.

Kwa mfano matatu ambazo zimekuwa zikilipisha Sh100 kati ya Nairobi na Kitengela, hivi sasa zinatoza Sh120-150.

“Kati ya saa kumi za jioni hadi saa moja, tutakuwa tukilipisha Sh150 lakini bei itabakia Sh100 baada ya saa mbili usiku,” akasema kondakta wa basi moja la kwenda Kitengela.

Alifichulia Taifa Leo Dijitali kuwa lengo kubwa la kupandisha nauli ni kufidia matumizi ili wasikadirie hasara, hasa wakati huu ambao mazingira ya biashara za usafiri ni magumu,

“Mwisho wa siku mpende msipende itabidi tujitahidi kwa sababu bado kampuni nyingi za bima huchukua hadi Sh10,000 kila mwezi na polisi vilevile wanahitaji chai,” akasema.

Kwingineko, nauli kati ya Nairobi na Nakuru imepanda kutoka Sh 400 hadi Sh600.

Kutoka Nairobi hadi Meru, wasafiri wengi wanalipishwa zaidi ya Sh 1,200 kinyume na bei ya awali ya Sh1,000.

Nakuru hadi Bungoma magari mengi ya uchukuzi yanatoza kati ya Sh 1,700 na 1,800  kinyume na bei ya awali ambayo ilikuwa Sh 1200 hadi 1500.?

Alfred Ambani mwendeshaji bodaboda eneo la Mlolongo anasema hii ni mara ya kwanza kwao kuongeza nauli kwa zaidi ya asilimia 20 kwa sababu pesa ambazo walikuwa wakipokea awali hazikuwa zikitosha.

Katika bei mpya ya mafuta jijini Nairobi petroli iliongezeka kwa zaidi ya Sh16, Dizeli Sh21 na mafuta taa Sh33

 

  • Tags

You can share this post!

Kuria amjibu Gachagua akijigamba yeye ndiye ‘truthful...

Maina Njenga alalamikia kudhulumiwa na ‘polisi’...

T L