• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 6:24 PM
Kondoo 50 walioibwa shamba la Kenyatta warejeshwa 

Kondoo 50 walioibwa shamba la Kenyatta warejeshwa 

Na SAMMY WAWERU 

KONDOO 50 kati ya 1, 500 walioibwa katika shamba la familia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wamerejeshwa.

Mwezi uliopita, Machi, wakati wa maandamano ya Azimio la Umoja kundi la wahuni lilivamia shamba la familia ya Bw Kenyatta, Northlands City lililoko eneo la Kamakis, Ruiru na kuiba mifugo hao.

Walikuwa wamejihami kwa mapanga na mashoka, ambapo waliiba kondoo bridi aina ya Dorper.

Shamba la Northlands City lilichomwa jioni ya Jumatatu, Machi 27, 2023. PICHA / SAMMY WAWERU

Duru zinaarifu kundi la kondoo hao 50 wa hadhi lilipatikana katika mojawapo ya mitaa Nairobi, kupitia minong’ono ya umma kwa askari na baada ya kuwakagua ilibainika ni wa Northlands City kufuatia alama ya utambulisho.

Aidha, inasemekana walirejeshwa katika makao yao kwa lori kwa njia ya siri.

Uvamizi wa shamba la familia ya Kenyatta ulifanyika wakati mmoja sawa na kampuni ya gesi (Spectre) ya kinara wa Azimio, Bw Raila Odinga.

Kiongozi wa Azimio la Umoja Bw Raila Odinga akizungumza katika shamba la Uhuru Kenyatta, Northlands City, lililovamiwa Jumatatu, Machi 27, 2023. PICHA / SAMMY WAWERU

Waziri Mkuu huyo wa zamani siku moja baada ya shamba la Kenyatta kuvamiwa, alilizuru na kukemea tukio hilo.

“Ni aibu sana mali ya Mkenya kuvamiwa na kuporwa, ilhali kuna serikali inayodai iko ange kulinda mali ya kila mwanachi,” Bw Odinga alisema, akikashifu baadhi ya viongozi na wanasiasa serikalini aliodai walikula njama kuvamia shamba la Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na mwenzake wa Kiharu, Ndindi Nyoro ni miongoni mwa aliotaja kiongozi huyo wa ODM.

Viongozi hao hata hivyo walijiondolea lawama, Ichungwa akiitaka idara ya polisi kufanya uchunguzi na kuchukulia hatua kisheria wahusika wa uvamizi huo.

Licha ya Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, IG, Japhet Koome kutangaza uchunguzi kuanzishwa hakuna yeyote aliyekamatwa.

Bw Kenyatta kufikia sasa hajaongea kuhusu uvamizi wa shamba la familia yake.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa kubaka akili punguani akiahidi kumpa chapatti...

Gavana Mung’aro apendekeza Mackenzie afungwe maisha

T L