• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 2:08 PM
Kuria amjibu Gachagua akijigamba yeye ndiye ‘truthful man’

Kuria amjibu Gachagua akijigamba yeye ndiye ‘truthful man’

NA RICHARD MAOSI

MALUMBANO makali yameibuka kati ya Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua na Waziri wa Biashara, Moses Kuria kila mmoja akionyesha ubabe wake.

Hali hiyo ya vuta nikuvute, inajiri kufuatia taarifa ya Bw Gachagua Jumapili, Septemba 17, 2023 iliyolenga Waziri Kuria – Naibu Rais akimkashifu kufuatia lugha yake chafu kwa wananchi.

Akimjibu, Bw Kuria ameashiria kujipiga kifua akidai kwamba yeye ndiye msema kweli – ‘truthful man’.

Kwa mara nyingine tena, katika hatua ambayo anaonekana kuenda kinyume na bosi yake, Kuria amefichulia taifa kuwa shehena ya mafuta iliyoagizwa Agosti itawasili nchini Oktoba, na ile ya Septemba itatua Novemba, bei mpya zikiwa zimeratibiwa.

Kupitia ujumbe aliopakia kwenye akaunti yake ya Twitter, Kuria ameelekeza msumari moto kwenye kidonda, baada ya kudai kwamba bei mpya za mafuta kati ya Septemba na Novemba zinajulikana.

Kuria ameungama kuwa ndiye mtetezi halisi wa Wakenya na kwamba amewaandaa wananchi kimawazo kwa hali ngumu ya maisha ambayo inakuja.

Naibu Rais Gachagua alikashifu matamshi ya Kuria akimtaka awe na nidhamu kwa waajiri wake ambao ni Wakenya.

Rigathi alisema anafuatilia kwa makini baadhi ya matamshi ya watumishi wa umma.

Kulingana na naibu rais, hakika wananchi wanaubeba mzigo mzito wa uchumi kutokana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na ongezeko la bei ya mafuta.

“Hali tunayopitia ya mfumko wa bei ya mafuta, si kero ya Kenya pekee ila ni ya kimataifa,” Bw Gachagua alisema kupitia taarifa mnamo Jumapili, baada ya kutua nchini kutoka Columbia.

Alikuwa amezuru Columbia kuhudhuria Maonyesho ya Kahawa.

Gachagua amewakanya viongozi hasa watumishi wa umma, akiwataka kupima maongezi yao kwa wananchi ambayo wakati mwingi huonekana kama ya kudunisha.

Aliongezea kuwa msururu wa madai ambayo yametajwa na Kuria siku za hivi karibuni na kuwaudhi Wakenya sio msimamo wa Rais William Ruto.

“Ingawa wananchi hawakuwateua moja kwa moja, waonyesheni heshima ambayo wanastahiki…Wao ndio waajiri wenu,” Gachagua alielezea.

Kando na kulenga Waziri Kuria, kauli ya Naibu Rais pia ililenga mshauri wa Rais Ruto kuhusu masuala ya uchumi, Bw David Ndii.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Khalwale ahimiza Ruto kufuta mawaziri wanaompotosha

Kondakta walia kulemewa kufikisha malipo ya siku kwa...

T L