• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:30 PM
Kutana na gavana mnyenyekevu zaidi nchini

Kutana na gavana mnyenyekevu zaidi nchini

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI wengi, hasa wale wa kisiasa nchini hupenda kujionyesha ni watu wa umaarufu, wenye nguvu na mamlaka kiasi kwamba lazima uwaone wakiwa na idadi kubwa ya walinda usalama wanaowazingira

Utampata Gavana, Mbunge, Seneta, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti au hata diwani nchini akiwasili mahali, iwe ni kwa hafla fulani ya kitaifa, kijamii au hata ile ya kawaida, akiwa ameandamana na misafara kadhaa, ikiwemo walinzi wengi wa kumjali na kumhakikishia kiongozi husika usalama wake.

Kwa gavana wa Lamu, Issa Timamy aidha, hali ni tofauti.

Utampata gavana huyo akiwa shughuli zake, akitembea wakati akitekeleza ukaguzi, iwe ni kwa mji wa kale wa Lamu au miradi mingine ile iliyoko kisiwani, iwe ni usiku au mchana bila ya kuandamwa na misafara mikubwa.

Yeye hutembea katika hali ya kawaida kinyume na viongozi wengine ambao lazima uwepo wao uuhisi wanapofika au kupita pahala popote.

Kwa gavana Timamy, mara nyingi watu, hasa wale wasiomjua au kumzoea, hujipata wakitagusana na kiongozi huyo bila hata kufahamu yupo.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo waliisifu tabia ya Bw Timamy ya kujinyenyekesha licha ya kuwa na cheo kikubwa anachohudumia kwa sasa cha kiongozi wa kaunti ya Lamu.

Bw Sharif Athman alimpongeza gavana Timamy kwa jinsi anavyojinyenyekesha, akiwasihi viongozi wengine nchini kuiga mfano wake.

“Mimi binafsi gavana Timamy ashawahi kunikaribia na kunisalimia nikiwa nimekaa na wenzangu barazani mjini Lamu. Kwa viongozi wengine, hilo halifanyiki. Hata kumkaribia na kumpa mkono ni ngumu. Wanaofanya hivyo wameishia kunyanyuliwa juujuu na kufurushwa na walinzi. Kwa gavana wetu, yeye ni mtu wa watu,” akasema Bw Athman.

Bi Fatma Ali alisema upendo alionao Bw Timamy kwa wananchi wake ndio umepelekea wengi kuvutiwa na yeye kiasi kwamba walinzi wawili au watatu anaoandamana naye hujipata wakiwa na kazi hafifu ya kumlinda kiongozi huyo wa kaunti.

“Utu wake umefanya wananchi kumpenda na kutagusana naye vyema. Wananchi wenyewe humpa gavana ulinzi. Wanatembea na yeye mitaani na hata kwenye vishoroba vya mji wa kale wa Lamu, wakimkinga na jazba zozote,” akasema Bi Ali.

Si kisiwani Lamu pekee ambapo Bw Timamy huwa na uhuru na watu wake na kutembea bila msafara wa walinzi.

Gavana wa Lamu Issa Timamy (kushoto) akiwa na maafisa wa usalama kisiwani Faza, Lamu mnamo Septemba 13,2023. PICHA | KALUME KAZUNGU

Utampata gavana Timamy akitembea kwa miguu, akisalimiana na watu kwenye visiwa vya Kizingitini, Faza, Mkokoni, Kiwayu, Kiunga na kwingineko.

Vile vile utampata akizungumza na wananchi, kutembea nao mitaani kwenye miji kama vile Mpeketoni, Witu, Hindi nakadhalika, kinyume na viongozi wengine waliowahi kuhudumia eneo hilo.

Licha ya Bw Timamy kuwa na gari maalum la kumsafirishia gavana sehemu mbalimbali kama magavana wengine nchini, yeye pia utampata akitumia magari ya kawaida pamoja na wananchi wakiingia kwa hafla mbalimbali, iwe ni za kijamii au za kiserikali.

Ugumu wa baadhi ya maeneo ya Lamu, hasa kimiundomsingi, ikiwemo barabara umesukuma magari makuukuu pekee kuhudumia maeneo hayo.

Bw Timamy katika harakati za kutoa huduma za kaunti maeneo hayo amekuwa akijitolea kusafiri, iwe ni kwa magari ya aina yoyote ilmradi afike eneo husika kuhudumia wananchi wake.

Licha ya Lamu kuwa na changamoto tele ya baadhi ya maeneo kama vile Lamu Mashariki, hasa kimiundomsingi, Bw Timamy yeye hajali kuyafika maeneo hayo kinyume na baadhi ya viongozi wengine ambao wamekuwa wakiyabagua licha ya kuyawakilisha.

Akizungumza kisiwani Faza, Lamu Mashariki hivi majuzi, Bw Timamy alisema atahakikisha maeneo ambayo yameachwa nyuma muda mrefu kimaendeleo anasukuma kupata maendeleo sawa na mengine eneo hilo.

“Kuna baadhi ya watu ambao hukereka wanaposikia mimi nimefika Lamu Mashariki kuhudumia watu wangu. Mimi nitawaambia kwamba ninayoyatekeleza yako kwenye katiba. Kwamba lazima maeneo yaliyoachwa nyuma kimaendeleo yapewe kipaumbele, kuzingatiwa ili yafikie usawa wa sehemu nyingine. Na ndiyo sababu mimi kila wakati mtanipata hapa Lamu Mashariki. Lazima maendeleo yafike eneo hili pia,” akasema Bw Timamy.

Bw Timamy ndiye gavana Mwanzilishi wa Lamu wakati ugatuzi ulipotwaa hatamu nchini mwaka 2013.

Mnamo 2017, Bw Timamy alikitetea kiti chake lakini akashindwa na mpinzani wake, Fahim Yasin Twaha.

Alijitosa tena ulingoni kutafuta kiti hicho kwenye Uchaguzi wa Agosti 9, 2022, ambapo alifaulu kumbwaga mrithi wake, Bw Twaha, hivyo kutwaa upya uongozi wa kaunti hiyo hadi wa leo.

Mbali na siasa, Bw Timamy pia ni wakili kitaaluma.

  • Tags

You can share this post!

Mwaka 1 hatujaonana na anadai ana mimba yangu

Kuria azidisha mashambulizi dhidi ya Gachagua

T L