• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
Macho yote kwa Spika Wetang’ula akitarajiwa kukabili kiazi moto cha Mswada wa Fedha 2023

Macho yote kwa Spika Wetang’ula akitarajiwa kukabili kiazi moto cha Mswada wa Fedha 2023

NA BENSON MATHEKA

HUKU makabiliano makali yakitarajiwa bungeni kuhusu Mswada wa Fedha 2023, ambao upinzani umekataa, macho yote sasa yanaelekezwa kwa Spika Moses Wetang’ula kuona iwapo atalinda uhuru wa Bunge.

Rais William Ruto amekuwa akishinikiza wabunge kupitisha mswada huo ambao unalenga kuongezea Wakenya mzigo wa ushuru na wafanyakazi kukatwa asilimia 3 ya mshahara kwa mfuko wa Ada ya Ujenzi wa Nyumba.

Kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga ameagiza wabunge wa muungano huo wa upinzani kukataa mswada huo ambao pia unalenga kuongeza ushuru wa VAT kwa mafuta kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16.

Wadadisi wa siasa wanasema mjadala kuhusu mswada huo tata unamweka Bw Wetang’ula kwenye darubini ilivyokuwa mtangulizi wake Justin Muturi, serikali ya Jubilee ilivyoshinikiza kupitishwa kwa sheria tata za usalama mwaka wa 2014.

Kwa wakati huu, Bw Muturi ndiye Mwanasheria Mkuu katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Kufuatia vitisho ambavyo Rais Ruto ametoa kwa wabunge na ikiwa wazi upinzani umepinga mswada huo, na ukiwa umekataliwa kwa wengi wa Wakenya, macho yote yatakuwa kwa Bw Wetang’ula kuona iwapo atalinda uhuru wa Bunge au ataruhusu uvurugwe na serikali kuu kutoka Ikulu,” akasema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Anasema kinachofanya Bw Wetang’ula kupigwa darubini kuhusiana na mswada huo ni tamko lake la kulaumu upinzani kwa kuukataa.

“Mheshimiwa, kuna joto jingi ambalo halina athari zozote. Kama rafiki yako, ninataka kukushauri kwamba usiogope kuchukua hatua au kuchukua hatua kwa kuogopa,” Bw Wetang’ula alimwambia Rais dakika chache kabla ya kiongozi wa nchi kuonya wabunge watakaokataa mswada huo.

Kulingana na Sheria ya Huduma ya Bunge ya 2019, na Kanuni za Bunge la Kitaifa, Spika hapaswi kuunga upande wowote katika masuala yote.

Kulingana na kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Bw Opiyo Wandayi, Bw Wetang’ula anafaa kusimama kidete kukataa serikali kuu kutisha wabunge kutokana na msimamo wao kuhusu Mswada huo.

“Kuna juhudi za kuingilia shughuli Bungeni na Wetang’ula anafaa kusimama kidete na kuilinda asasi hiyo isivamiwe,” alisema Bw Wandayi.

Kulingana na Dkt Gichuki, uongozi wa Wetang’ula katika Bunge la Kitaifa unawekwa kwenye mizani kwa kuwa ni mmoja wa vinara wa Muungano wa Kenya Kwanza ambao ulimteua na kuhakikisha anatwaa wadhifa wa Spika.

“Hata kama alijiuzulu kama kiongozi wa chama chake, ukweli unakabakia kwamba Wetang’ula ni kinara wa Kenya Kwanza na utendakazi wake utafuatiliwa kwa makini hasa kuhusiana na mswada huu tata wa Fedha 2023.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah anasema Bw Wetang’ula alipaswa kukemea matamshi ya viongozi wa serikali ya kutisha wabunge ili waunge mswada huo.

Spika huyo alihudhuria mkutano wa maombi ambao Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua walitisha wabunge ili kuwashinikiza kuunga mswada huo.

“Wetang’ula hawezi kusimamia taasisi ambayo inashambuliwa na kisha aunge wanaofanya hivyo,” Bw Omtatah alinukuliwa akisema.

  • Tags

You can share this post!

Sakata ya Kemsa: Terry Ramadhani adai waziri Nakhumicha...

Enyi kina Brayo na Jayden, mkienda Lamu mtakosa majina!

T L