• Nairobi
  • Last Updated March 4th, 2024 8:55 PM
Machogu: Usahihishaji KCPE ulikuwa kazi safi na wakuu wa shule wameridhika na walichopata

Machogu: Usahihishaji KCPE ulikuwa kazi safi na wakuu wa shule wameridhika na walichopata

NA TITUS OMINDE

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amepuuzilia mbali madai ya kasoro katika usahihishaji wa mtihani wa KCPE mwaka huu huku akipongeza maafisa wake kwa kutenda kazi njema.

Akizungumza katika taasisi ya mafunzo anuai ya Eldoret National Polytechnic wakati wa hafla ya kufuzu ya 18, Bw Machogu alisifu jinsi mtihani ulivyosahihishwa, akisisitiza kwamba waliosahihisha walifanya kazi nzuri.

Bw Machogu alidai kuwa hitilafu chache zilizoshuhudiwa wakati wa uwekaji alama zilitokana na changamoto za kiufundi ambazo ni za kawaida.

“Usahihishaji wa KCPE uliomalizika hivi punde ulikuwa mzuri, nina maafisa waliohitimu ambao walifanya kazi nzuri wakati wa uwekaji alama, na changamoto chache ambazo zilishuhudiwa zilitokana na hitilafu za kiufundi ambazo zitatatuliwa hivi karibuni,” alisema Bw Machogu.

Kulingana na Bw Machogu, madai ya kusahihishwa vibaya kwa mtihani huo hayana msingi ambapo alisema maafisa wa KNEC na wataalamu kutoka wizara ya elimu iko tayari kudhihirisha kamati ya bunge kuhusu elimu jinsi zoezi hilo lilivyofanywa kwa njia bora.

Bw Machogu aliwapongeza maafisa waliohusika katika kusahihisha mtihani huo kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Waziri huyo alisisitiza kuwa shughuli nzima ya kutia alama ilikuwa kamilifu licha ya malalamiko kutoka kwa watahiniwa na wazazi kutoka maeneo tofauti nchini.

Alisema kuwa matokeo ya mitihani yaliyoonyeshwa katika tovuti ya KNEC yalikuwa bora na changamoto ziliibuka kutokana na uwasilishaji.

“Tulipotoa mtihani, kila kitu kilikuwa sawa na Wakuu wa Shule mbalimbali wanaweza kuthibitisha kwamba matokeo katika tovuti ya KNEC kwa shule yalikuwa kamili, katika uwasilishaji kulikuwa na hitilafu za kiufundi,” alisema Bw Machogu.

Aliondoa hofu yoyote kabla ya matokeo ya KCSE akisema kuwa kila kitu kiko sawa na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.

Akijibu hoja za Mbunge wa Kesses Julius Rutto aliyesema kuwa matukio yalifuata baada ya kutangazwa kwa mtihani huo wa KCPE 2023 yanatia doa uadilifu wa KNEC .

“Matokeo ya hivi majuzi ya KCPE ambapo wanafunzi wengi hawakuridhishwa na jinsi mtihani ulivyosahihishwa yanaweka uadilifu wa baraza la mitihani hatarini na lazima wizara ijieleze waziwazi kuhusu suala hilo tunapotarajia matokeo ya KCSE kufikia mwisho wa mwezi huu,” akasema Bw Rutto.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Rose Muhando akanusha kutapeli kanisa la mwimbaji Mkenya...

Harambee Starlets warejea kimya kimya baada ya kukosa fursa...

T L