• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Mackenzie hubomoa chakula sawasawa akiwa kizuizini, serikali yasema

Mackenzie hubomoa chakula sawasawa akiwa kizuizini, serikali yasema

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA mkuu wa mauaji ya halaiki ya Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Bw Paul Mackenzie, amekuwa akihamishwa kutoka seli ya kituo kimoja cha polisi hadi kingine ili asikabwe na njaa, serikali imedai.

Katika mawasilisho mahakamani Shanzu, upande wa mashtaka ukiongozwa na Bw Jami Yamina, ulisema kumekuwa na changamoto kumlisha Bw Mackenzie na washukiwa wenzake 30 kila siku ndiposa wamekuwa wakihamishwahamishwa.

Alieleza hayo baada ya mawakili wa washtakiwa kulalamika kwamba, wakati mwingine huwa wanaenda kituo fulani cha polisi kuwaangalia lakini wanapata walihamishwa.

“Walihamishwa kwa sababu ya masuala ya chakula. Chakula kilikuwa kimeisha hivyo ilitubidi kuwahamishia mahali ambapo wangeweza kupata chakula,” akasema Bw Yamina.

Washukiwa hao siku za nyuma walilalamikia uhaba wa chakula wakilalamikia kupewa supu ya maharage pekee wakiwa kizuizini.

Siku ya Ijumaa kabla ya kesi kuanza, Mackenzie aliwaomba wanahabari kwa mzaha wamnunulie maziwa na mkate.

“Nyinyi wanahabari senti mmeunda na hata hamuwezi kuninunulia mkate. Mimi nimekaziwa hapa hata siwezi kupata pesa. Si muende muniletee angalau paketi ya maziwa,” alisema Mackenzie.

Mawakili wa washtakiwa, Bw Elisha Komora, Bw Wycliffe Makasembo na Bw George Kariuki, walikuwa wameeleza hofu kuwa serikali inataka kukatiza juhudi zao za kuwatembelea na kuzungumza na washukiwa.

“Nilizuru kituo cha polisi cha Malindi nilipokuwa nikielekea Lamu lakini nikakuta washukiwa wamehamishwa hadi kituo tofauti cha polisi. Serikali inastahili kutufahamisha wakati wa kuwahamisha washukiwa hao ili tusipoteze muda na pesa kuzuru vituo vya polisi na kuwakosa,” akasema Bw Komora.

Wakati huo huo, washukiwa walilalamikia hali ngumu ya maisha rumande wakisema hawajabadilisha nguo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

“Nimeambiwa na washukiwa kwamba wapelelezi sasa wameanza kuwatesa kisaikolojia na kimwili. Hii ni kinyume na sheria,” alisema Makasembo.

Alidai kuwa, kuna wapelelezi waliojaribu kuwalazimisha baadhi ya washukiwa kusaini hati za kukiri kosa kuhusiana na matukio ya Shakahola.

Lakini Bw Yamina alipinga madai hayo akisema kuwa tuhuma hizo ni nzito na zinapaswa kuwasilishwa mahakamani kwa njia ya hati ya kiapo inayoambatanisha ushahidi wa kuunga mkono madai hayo.

Pia, washukiwa hao walidai kuwa walikuwa wakinyimwa faragha hata wakati wa kuenda msalani kujisaidia.
Walidai kuwa polisi walikataa kutoa pingu walizofungwa na kuwalazimisha kuenda msalani wawili wawili.

“Tunafungwa pingu hata tunapoenda haja. Inabidi twende huko wawili wawili,” walilalamika.

Idadi ya washukiwa ambao wanazuiliwa kuhusiana na maafa ya Shakahola sasa imefikia 31 baada ya washukiwa wengine 13 kunyakwa.

Hata hivyo, mmoja kati ya washukiwa 13 wapya ameonyesha nia ya kuwa shahidi ya upande wa mashtaka.

Bw Mackenzie na wenzake wanachunguzwa kwa makosa ya kusaidia watu kujiua, mauaji, utekaji nyara, utoaji mafunzo ya itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu na ukatili wa watoto. Kesi hiyo itatajwa tena Juni 7.

  • Tags

You can share this post!

ODM wamchoka Owalo na misaada yake ya chakula Luo Nyanza

Bado nasubiri jibu la demu miaka 2 sasa!

T L