• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Madampo kila kona yaharibu sura ya Nairobi

Madampo kila kona yaharibu sura ya Nairobi

NA SAMMY KIMATU

WAENDESHAJI magari na wanaotembea kwa miguu kando ya barabara kadhaa jijini Nairobi wamekerwa na ongezeko la madampo ya taka.

Waliozungumza na Taifa Leo wanasema kwamba taka hizo huhatarisha afya za watu na kudunisha hadhi ya jiji la Nairobi.

Mojawapo ya maeneo hayo ni kando ya daraja la Reuben mkabala wa barabara ya Enterprise, makutano ya barabara ya Enterprise/Likoni na Steji ya Kayaba.

Maeneo mengine ni steji ya Busia, makutano ya barabara ya Dar es Salaam/Dakar na mita chache karibu na steji ya City Stadium kutokea DT Dobie.

Aidha, wanaomba mwanakandarasi aliyepewa kazi na serikali ya kaunti kuzoa uchafu huo kabla ya kuripotiwa kwa mkurupuku wa magonjwa.

“Uvundo kutoka kwa madampo hayo huingia hadi ndani ya matatu,” Bw Simon Maina anayehudumu Indimanje Sacco akasema.

Waliozungumza na Taifa Leo walihoji kwamba nyingi ya taka hizo humwagwa usiku na watu wanaotumia mikokoteni.

“Ni vigumu kuona watu wakimwaga taka mchana. Mara nyingi humwagwa usiku na watu wanaozileta wakitumia mikokoteni,” mlinzi katika kiwanda kimoja mkabala wa barabara ya Busia akasema.

Mhandisi kutoka kwa serikali ya kaunti ambaye alidinda kutajwa jina aliwalaumu wanaochafua maeneo hayo akisema hayatambuliwi na kaunti kama maeneo ya kutupa taka.

“Katika maeneo yaliyotambulikana na serikali ya kutupa taka, malori ya wakandarasi huja kubeba taka hizo na kuzipeleka Dandora. Wanaomwaga taka usiku wanatakikana kukamatwa kwa sababu huu ni uhalifu na lazima kanuni za jiji zifuatwe kwa mujibu wa sheria,” mhandisi huyo akadokeza.

Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kwamba hakuna sehemu iliyotengwa mahususi kwa umwagaji wa taka katika Eneo la Viwanda lililo na shughuli nyingi.

Tingatinga la kuzoa taka karibu na steji ya Kayaba kwenye barabara ya Enterprise Road jijini Nairobi. PICHA | SAMMY KIMATU

Vile vile, nyingi ya taka hizo hutoka kwa wachuuzi walio na vibanda karibu na steji za magari japo kuna wale huwapa vibarua kazi ya kukusanya taka mitaani bila kujali taka hizo humwagwa wapi.

“Katika hii steji ya Kayaba na ile ya Busia, kuna wale ambao huwapatia vijana Sh20 na kuwaambia waondoe taka jioni baada ya kufunga maduka au vibanda vyao vya mboga. Baadaye vibarua hao ndio hutupa ovyo taka walizokusanya mitaani,” Bw Urbanus Ngila Mwau, kiongozi wa walemavu Kayaba na kadhalika mwenyekiti wa wafanyabiashara wa juakali Busia Road akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Waziri Kindiki: Shakahola ina makaburi mengi

Waliovamia shamba la familia ya Uhuru Kenyatta kukamatwa

T L