• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Madaraka Dei: Viti vingi vyakosa wa kuvikalia uwanjani KMTC Siaya

Madaraka Dei: Viti vingi vyakosa wa kuvikalia uwanjani KMTC Siaya

NA KASSIM ADINASI

WAKAZI wachache wa Kaunti ya Siaya wamejitokeza katika uwanja wa KMTC kuadhimisha makala ya 60 ya Madaraka Dei, sherehe ambazo zimeadhimishwa kote nchini Kenya.

Waliohutubu uwanjani KMTC wameitaka serikali na viongozi kuwawezesha zaidi wanawake na watu wanaoishi na ulemavu.

Baadhi ya viti uwanjani humo vilisalia wazi kutokana na idadi ya chini ya waliojitokeza.

Kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga anatoka Bondo katika Kaunti ya Siaya. Hakuna kiongozi yeyote aliyechaguliwa ambaye amehudhuria sherehe hizo.

Hata hivyo, maafisa wa serikali wamehudhuria. Mawaziri wawili kotoka serikali ya kaunti ambao ni Agunda Ochanda (uongozi) na Dkt Martin Konyango (Afya), Mkuu wa Wafanyakazi Cyrus Oguna ndio maafisa wa pekee kutoka kwa serikali ya Gavana James Orengo ambao wamehudhuria sherehe hiyo.

Kupitia kwa hotuba yake iliyosomwa na Bw Ochanda, Gavana Orengo ameahidi kuendelea kuhakikisha wakazi wanafurahia utawala bora.

Naye Dkt Konyango amewataka wakazi wajisajili kwa mpango wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) wanufaike na matibabu ya gharama ya chini.

“Ninahimiza nyini wakazi mchukue bima ya afya ili mpate huduma za msingi katika vituo vya afya vya umma. Inasikitisha kwamba watu wengi huhangaika kwa kushindwa kulipa bili za matibabu hospitalini,” amesema Dkt Konyango.

Viongozi wengine waliopata fursa ya kuhutubu wamehimiza haja ya kuwawezesha zaidi wanawake katika jamii.

“Ukimuelimisha mwanamke, umeelimisha jamii nzima. Hizi si zama za wanawake kuonekana tu kama chanzo cha mahari,” amesema Profesa Achola Wao, ambaye ni Mwenyekiti wa Manispaa ya Siaya.

Kauli yake imeungwa mkono na mwenyekiti wa tawi la Siaya la chama cha Maendeleo ya Wanawake Bi Pattricia Apoli na diwani maalum Profesa Jacklyn Oduol.

“Sababu zinazoyumbisha elimu ya mtoto wa kike kama mimba za mapema ni sharti zikabiliwe vilivyo na wanaume na wanawake kwa pamoja,” amesema Bi Apoli.

  • Tags

You can share this post!

Madaraka Dei 2023: Rais Ruto aahidi kuzindua bodaboda...

FKF yashirikiana na FIFA kukuza soka ya akina dada nchini

T L