• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Mahabusu wakodolea macho njaa serikali ikifilisika

Mahabusu wakodolea macho njaa serikali ikifilisika

Na JUSTUS OCHIENG

MAHABUSU waliozuiliwa katika seli za polisi wako katika hatari ya kukosa chakula baada ya vituo vya polisi kuishiwa na fedha.

Wasimamizi wa vituo vya polisi wamelazimika kukopa fedha ili kuendesha shughuli.

Wakuu wa polisi waliozungumza na Taifa Leo walielezea jinsi wanavyolazimika kutumia hela zao kununua mafuta ya magari ya kushika doria.

Afisa wa ngazi ya juu katika makao makuu ya polisi katika Jumba la Vigilance, alifichua kuwa baadhi ya wanakandarasi ambao wamekuwa wakisambaza vyakula katika vituo vya polisi ili kulisha mahabusu wametishia kuacha kutoa huduma hiyo kwa kutolipwa.

Baadhi ya wanakandarasi hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miezi 10.

Mkuu wa polisi katika kituo kimojawapo jijini Nairobi alidokeza kuwa maafisa wa usalama watagoma kushika wahalifu na kuwazuilia katika seli za polisi kwani hawawezi kutumia fedha zao kulisha mahabusu.

Alisema polisi wamekuwa wakilazimika kukodisha teksi kwa kutumia fedha zao kupeleka washukiwa kortini kwani magari ya serikali hayana mafuta.

“Ninatumia hela zangu kununua karatasi za kuandikia mashtaka kabla ya kupeleka mahabusu kortini kwa kutumia teksi,” akasema afisa huyo.

Mvutano kati ya Idara ya Polisi na Wizara ya Usalama wa ndani kuhusu udhibiti wa fedha umesababisha vituo vya polisi kukosa fedha za kuendeshea shughuli.

Mara baada ya kuapishwa mwaka jana, Rais William Ruto alipokonya wizara ya Usalama jukumu la kudhibiti fedha za Idara ya Polisi.

Badala yake, Dkt Ruto alimtwika Inspekta Jenerali Japhet Koome jukumu la kudhibiti fedha za idara hiyo.

Agizo hilo la Rais limesababisha mvutano baina ya taasisi hizo mbili. Polisi wanasema hawajapokea fedha za kuendeshea vituo kwa zaidi ya miezi sita iliyopita.

Juhudi za Taifa Leo kupata taarifa kutoka kwa Bw Koome, naibu wake Noor Gabow, Waziri wa Usalama Kithure Kindiki na Katibu wa Wizara ya Usalama, Dkt Raymond Omollo ziligonga mwamba kwani hawakujibu simu.

  • Tags

You can share this post!

Waititu amezirai nyumbani, wakili aambia korti katika kesi...

Mswada wa ushuru: Raila kutoa mwelekeo Alhamisi

T L