• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Mahakama ya juu yaombwa iruhusu mpango wa BBI wa kubadilishha katiba uendelee

Mahakama ya juu yaombwa iruhusu mpango wa BBI wa kubadilishha katiba uendelee

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Juu jana ilianza kusikiza rufaa ya mpango wa kubadilisha katiba (BBI) huku Mwanasheria Mkuu Bw Paul Kihara akiteta kwamba mahakama ya rufaa na mahakama kuu zilipotoka zilipositisha hatua ya kubadilisha katiba.

Jaji Mkuu Martha Koome , Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala , Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko waliombwa waruhusu mpango wa kubadilisha katiba uendelee.

Mahakama hii ya upeo iliombwa ifutilie uamuzi wa mahakama ya rufaa kwamba Rais anaweza kushtakiwa akiwa angali afisini, kwamba tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC haikuwa na makamishna wa kutosha ilipoidhinisha mpango wa BBI.

Pia mahakama hii ya upeo iliombwa iruhusu mpango wa BBI uendelee na kwamba maoni ya wananchi yalishirikishwa kabla ya hoja ya kubadilisha katiba kujadiliwa na mabunge ya kaunti. Wakili Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto pamoja na mawakili George Oraro na Kamau Karori wanaomwakilisha Bw Kihara waliwasihi majaji hao watupilie mbali maamuzi yaliyoruhusu Rais awe akishtakiwa akivunja sheria na akitoa maamuzi potovu.

“Naomba hii mahakama itupilie maamuzi kwamba Rais anaweza shtakiwa angali afisini. Ni kinyume cha sheria,” Bw Karori alisema alipotoa mawasilisho mbele ya Jaji Koome. Bw Karori alisema Kifungu nambari 142 kinapinga mtu yeyote kumfungulia Rais mashtaka kutokana ana maamuzi anayochukua akiwa afisini.

Akisema Rais hapotezi haki za kushiriki katika masuala ya uchaguzi anaposhika hatamu za uongozi, Bw Karori alisema Rais Uhuru Kenyatta hakuvunja sheria alipoongoza mchakato wa kubadilisha katiba. Majaji hao walielezwa majukumu ya Rais yameelezwa katika katiba ikiwa ni pamoja na kutoa mwelekeo katika masuala mbali.

“Kushiriki kwa Rais Kenyatta katika mchakto wa BBI hakukuwa kinyume cha sheria hata!,”Bw Karori alisisitiza. Bw Karori alisema Rais anatakiwa kuhakikisha usalama upo nchini na hakuna jambo linaloathiri wananchi ikiwa ni pamoja mashambulizi kutoka mataifa ya kigeni.

Prof Githu Muigai aliomba uamuzi IEBC haikuwa na makamishna wakutosha ilipoidhinisha mchakato wa kubadilisha katiba uendelee na kupelekwa kujadiliwa katika mabunge ya kaunti. Prof Muigai aliomba mahakama hii ya upeo iamuru makamishna watatu wa IEBC walioidhinisha mchakato wa BBI na kukagua sahihi milioni moja za wapiga kura ilikuwa idadi tosha.

Mahakama ya rufaa na Mahakama kuu zilisema IEBC haikuwa na idadi ya kutosha ilipoidhinisha mchakato wa BBI kuendelea. Mahakama hizo zilisema katika maamuzi kwamba idadi ya makamishna wa IEBC iliyotakiwa kuidhinisha mchakato wa BBI ni watano.

Lakini Prof Muigai alisema IEBC ilikubaliwa na majaji wawili wa mahakama kuu kuendeleza shughuli zake ikiwa na makamishna watatu. Kesi inaendelea

You can share this post!

Chama cha Kingi chazidi kupondwapondwa kutoka pande zote

Mdalasini na faida zake mwilini

T L