• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Mahakama yaipiga breki serikali kuuza KICC, mashirika mengine 10

Mahakama yaipiga breki serikali kuuza KICC, mashirika mengine 10

NA SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA Kuu imesitisha kwa muda mpango wa serikali kuuza mashirika 11 ikiwemo jengo la Mikutano ya Kimataifa la KICC na kampuni ya Kenya Pipeline Company (KPC) baada ya kesi kuwasilishwa na chama cha Raila Odinga cha Orange Democratic Movement (ODM).

Jaji Chacha Mwita ameamuru kwamba masuala yaliyoibuliwa na ODM yanaangazia masuala nyeti ya kikatiba na kisheria ambayo yana umuhimu mkubwa kwa umma na hivyo ni muhimu yaangaziwe kwa umakini mkubwa na mahakama.

Jaji Mwita ameamuru ODM kumkabidhi Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u nakala za kesi hiyo bila kupoteza muda.

“Agizo la muda linatolewa kuzima utekelezaji wa kipengee 21(1) cha Sheria ya Ubinafsishaji ya 2023 na au uamuzi wowote uliofikiwa hadi Februari 6, 2024,” jaji Mwita amesema kwenye uamuzi wake.

Chama cha ODM kinadai katika kesi hiyo kwamba mashirika yanayotaka kuuzwa ni ya umuhimu mkubwa kwa Wakenya na hivyo yanaweza yakauzwa tu ikiwa raia wenyewe wametoa idhini kupitia kwa kura ya maamuzi yaani refarenda.

Mashirika ambayo serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto inapanga kuuza ni KICC, KPC, kampuni ya maziwa ya New Kenya Cooperative Creameries (New-KCC), shirika la uchapishaji la Kenya Literature Bureau (KLB), shirika la mafuta la National Oil Corporation of Kenya (NOCK) na kampuni ya mbegu ya Kenya Seed Company Limited (KSC).

Mengine ni Mwea Rice Mills Ltd (MRM), Western Kenya Rice Mills Ltd (WKRM), Numerical Machining Complex Limited (NMC), Kenya Vehicle Manufacturers Limited (KVM) na kiwanda cha nguo cha Rivatex East Africa Limited (REAL) kinachomilikiwa na Chuo Kikuu cha Moi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ndege yapata panchari ikitaka kupaa Manda

Jamaa wa wanaume sita walioshtakiwa kwa wizi wa Sh94...

T L