• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Maina Njenga aachiliwa kwa dhamana wakili wake akidai anaandamwa kisiasa

Maina Njenga aachiliwa kwa dhamana wakili wake akidai anaandamwa kisiasa

NA MERCY KOSKEI

MAHAKAMA ya Nakuru imemwachilia aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga kwa bondi ya sh100, 000 au dhamana ya Sh50, 000 pesa taslimu.

Alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Kipkurui Kibelyon mnamo Jumatatu, Mei 29, 2023 Njenga alipinga makosa saba aliyokuwa ameshtakiwa nayo.

Anatuhumiwa kuwa mwanachama na kiongozi wa genge lililopigwa marufuku la Mungiki na kushiriki kupanga shughuli za uhalifu katika nyumba yake iliyoko Wanyororo, Kaunti ya Nakuru, Mei 12, 2023.

Njenga pia anadaiwa kuhutubia mkutano katika eneo hilo la Wanyororo, akihimiza “uungwaji mkono” kwa baadhi ya waliokuwemo kurejea kujiunga na kundi hilo haramu la Mungiki.

Martha Karua, alipowakilisha aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga kama wakili wake mahakamani Nakuru. Picha / RICHARD MAOSI

Kulingana na nakala za mashtaka, Njenga alikuwa ameshtakiwa na washukiwa wengine 11 waliopatikana nyumbani kwake Wanyororo.

Vile vile, kiongozi huyo wa zamani wa kundi hilo haramu, anadaiwa kupatikana na rekodi zinazoweza kuwa na manufaa kwa mtu anayejiandaa kutekeleza uhalifu unaohusisha genge la Mungiki.

“Washtakiwa walipanga na kuhudhuria mkutano pamoja na wengine, ambao madhumuni yake yalikuwa kuhimiza uungwaji mkono kwa genge la Mungiki,” ilieleza sehemu ya nakala ya mashtaka.

Inadaiwa aliwaalika washtakiwa wenza katika mkutano huo, alioongoza nyumbani kwake na akauruhusu kuendelea kinyume na sheria licha ya kujua kuwa ni kampeni ya kukuza genge hilo.

Hata hivyo, Wakili wa Njenga Bi Martha Karua, aliiomba mahakama kumwachilia kwa masharti ya bondi au kwa njia mbadala, bondi ya bure.

Bi Karua alisisitiza kuwa Njenga hatakosa kufika mahakamani wakati anapohitajika kwani alijisalimisha mbele ya mahakama na mbele ya maafisa wa upelelezi wa jinai (DCI) alipohitajika.

Maafisa wa polisi wakishika doria Maina Njenga alipofikishwa kortini Nakuru kufuatia mashtaka yanayomuandama kufufua kundi haramu la Mungiki. Picha / RICHARD MAOSI

Alidai pia kuwa Njenga hakuwa na hatia na mashtaka yanayomuandama yalichochewa kisiasa.

Akimwachilia kwa dhamana, Hakimu Kibelyon alionya Njenga kutojaribu kutoa matamshi kupitia vyombo vya habari au mikutano ya hadhara ambayo ina marejeleo ya kesi hiyo.

Mahakama pia iliamuru kwamba asifanye mawasiliano na mashahidi wowote wa upande wa mashtaka kwa njia ambayo huenda ikatatiza kesi hiyo.

Alisema ukiukaji wowote wa maagizo hayo yatasababisha kufutwa kwa dhamana inayomwakilisha kuachiliwa.

“Mshtakiwa anaweza kuachiliwa kwa dhamana. Hafai kuzungumzia kesi iliyoko mahakamani kwa vyombo vya habari au mahala popote,” aliamuru.

Kesi hiyo itatajwa Juni 20.

 

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yaidhinisha wakili Mitchell Kemuma kuwa MCA maalum...

Museveni asaini mswada ambao unapinga ushoga

T L