NA SAMMY WAWERU
ALIYEKUWA Kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga amezungumza kwa mara ya kwanza tangu taarifa za kutekwa nyara kwake zifichuke.
Bw Njenga, ambaye pia ni pasta alikamatwa mnamo Jumamosi, Septemba 17, 2023 na watu wasiojulikana.
Alitekwa nyara akiwa pamoja na msaidizi wake, Felix Lakishe.
Mwanasiasa huyo, hata hivyo, alipatikana Jumatatu, Septemba 18, 2023 katika hali isiyoeleweka ambapo aliwasilishwa katika Mahakama ya Makadara, Nairobi.
Ana kesi inayomkabili, anayotuhumiwa kwa kupatikana na silaha hatari kwenye nyumba zake wakati wa maandano ya Azimio.
Akihutubia wanahabari nje ya korti Makadara, Bw Njenga alidai kwamba alitekwa nyara na askari.
“Wasidhani hatujui waliotukamata; ni askari,” alisema.
Alikuwa ameandamana na wakili wake, Ndegwa Njiru, pamoja na wanafamilia na baadhi ya wafuasi wake wa karibu.
Kulingana na Bw Njenga, waliomkamata walikuwa wameficha nyuso zao – kujifunga ili wasitambulike.
Alilalamikia kuteswa na kuhangaishwa, akisema hawakupelekwa katika kituo chochote cha polisi.
“Hatujui tulikokuwa…Tulipitia dhuluma na mateso,” alisimulia, akielezea kushangazwa kwake haki zake Kimsingi na Kikatiba kuhujumiwa.
“Hii ni nchi yenye sheria, tulitoka kwa utawala wa kiimla, kidikteta na wa kimabavu.”
Kuachiliwa kwake pia kunajiri baada ya mrengo wa upinzani ukiongozwa na kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua kukashifu vikali kutekwa nyara kwake.
Azimio aidha inalalamikia kuhangaishwa na serikali ya Rais William Ruto, wakati ikitetea Wakenya gharama ya juu ya maisha ishushwe.