• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Maina Njenga asema watekaji nyara walimpa yeye na msaidizi wake Sh2,000 za nauli

Maina Njenga asema watekaji nyara walimpa yeye na msaidizi wake Sh2,000 za nauli

NA CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga mnamo Jumatatu, Septemba 18, 2023, alielezea masaibu yake mikononi mwa watu wasiojulikana waliomteka nyara kutoka nyumbani kwake, kaunti ya Kiambu siku ya Jumamosi, Septemba 16, 2023.

Akiongea na wahabari nje ya Mahakama ya Makadara jijini Nairobi, Bw Njenga alifichua kuwa aliachiliwa huru na watekaji wake muda mfupi baada ya saa nne usiku mnamo Jumapili.

Alidai kuwa waliomteka, pamoja na msaidizi wake Felix Lekishe, walikuwa ni maafisa wa usalama waliokuwa na silaha.

“Tulifungiwa ndani ya chumba kidogo ambacho hakikuwa na taa,” akasema.

Baada ya kusalia chumbani humo kwa saa 24, Bw Njenga akasema, walisafirishwa kwa gari kwa karibu saa mbili na kuachwa katika mtaa wa Banana, ambako walipewa Sh2,000 wakatumie kama nauli ya kuenda nyumbani.

Bw Njenga alisema aliabiri pikipiki ya uchukuzi almaarufu kama bodaboda na kuelekea nyumbani.

Kiongozi huyo wa zamani wa Mungiki alisema hayo baada ya kufika mahakamani kuhudhuria kikao cha kusikilizwa kwa kesi dhidi yake ya kumiliki silaha haramu.

Bw Njenga, ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya, aliachiliwa huru baada ya vinara wa muungano huo kulaani kutekwa nyara kwake na kuelekeza kidole cha lawama kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Wakiongea na wanahabari mnamo Jumapili jioni katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga zilizoko katika mtaa wa Upper Hill, vinara wa Azimio Kalonzo Musyoka na Martha Karua walidai polisi jeuri ndio waliomteka nyara Bw Njenga.

  • Tags

You can share this post!

Mwili wa mwanamume wafukuliwa kinyume na itikadi za...

Jinsi mwanafunzi wa kike alivyoporwa na wanaume wawili...

T L