• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Majonzi, hasara mvua ikiendelea kushuhudiwa nchini   

Majonzi, hasara mvua ikiendelea kushuhudiwa nchini  

BRIAN OCHARO, CECE CIAGO, BENSON MATHEKA, STEPHEN ODUOR NA WINNIE ATIENO

WAFANYAKAZI wawili wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) ambao walisombwa na mafuriko Ijumaa walipokuwa wakivuka daraja la Ramisi, Lungalunga, Kaunti ya Kwale, wametambuliwa huku mvua kubwa ikitarajiwa kuendelea kote nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Mipaka ya Lungalunga, Bw Joram Maina na mwenzake Bw David Ng’ang’a, walikumbana na kifo chao gari aina ya Land Cruiser walimokuwa wakisafiria liliposombwa na maji ya mafuriko katika Mto Ramisi.

Gari hilo liliopolewa mtoni Jumamosi na kuburutwa hadi kituo cha polisi cha Msambweni.Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Dkt Raymond Omollo, alifichua majina ya marehemu na kuzihakikishia familia zao kwamba timu ya mashirika mbalimbali tayari ilitumwa katika eneo la tukio ili kusaka miili yao.

“Timu ya mashirika mengi inayoongozwa na Kenya Coast Guard iko kwenye eneo la tukio kujaribu kutafuta miili. Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia na marafiki wakati huu mgumu,” Dkt Omollo alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Kufikia saa saba mchana, miili ya watu watatu illikuwa imepatikana.

“Bado hatujatambua ikiwa ni ya meneja au dereva wake. Mchakato wa kutambua miili hiyo inaendelea,” Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Bw Michael Meru, alisema.

Maafisa hao wawili walikuwa wakisafiri Mombasa kutoka Lunga Lunga Ijumaa walipokumbana na mauti.

Wakati huo huo, mwili wa mwendeshaji bodaboda mwenye umri wa miaka 23, ambaye pia alisombwa na maji katika eneo moja, umepatikana katika eneo hilo hilo.Jana, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema Mvua ya El Nino inayoendelea kunyesha nchini imeathiri watu 80,000 katika kaunti 33.

Bw Gachagua alisema kwa wiki moja iliyopita, kaunti zilizoathiriwa zimeongezeka kutoka 19 hadi 33 na idadi inatarajiwa kuongezeka ikizingatiwa mvua inaweza kuendelea hadi Desemba na Januari.

Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, amelilia wahisani kuingilia kati kuwasaidia waathiriwa kwa fedha na chakula.Akizungumza na Taifa Leo, msemaji wa serikali ya kaunti hiyo, Bw Nicky Gitonga, alisema takwimu kutoka kwa wasimamizi wa wadi zote, zilifichua takriban watu saba wamepoteza maisha kutokana na mvua ambayo inaendelea kunyesha katika eneo la Pwani huku mamia ya nyumba zikiharibiwa.

“Tuna zaidi ya watu 5,000 ambao wameathiriwa. Gavana anaomba msaada kwa wahisani kuja kutusaidia,” alisema na kuongeza kuwa wadi 10 kati ya 20 za kaunti hiyo, zimeathiriwa na mafuriko.

Katika kaunti ya Tana River, siku 21 zilizopita zimekuwa mbaya kwa waathiriwa wa mafuriko. Baridi, njaa, na magonjwa yamekuwa yakipiga hodi.

“Niliweza kuokoa kitu kimoja tu mafuriko yalipokuja, nilichagua watoto wangu na kutazama kila kitu kingine kikienda na maji pamoja na nyumba yangu,” Bi Halima Barisa, mwathiriwa alisema.

Alikimbilia kwenye nyumba ya rafiki yake pamoja na watoto wake wanne na amekuwa akistahimili baridi kali na mbu kwa wiki mbili.

  • Tags

You can share this post!

Mbinu maalum anayotumia mfugaji kupata malisho eneo kame...

Wizi wa punda Nyandarua waanza, Nairobi ikiwa soko kubwa la...

T L