• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Maseneta wamkataza gavana kutengenezea mke wake ofisi

Maseneta wamkataza gavana kutengenezea mke wake ofisi

NA MARY WANGARI

BUNGE la Kaunti ya Kakamega limeshutumiwa kwa kujishughulisha na uundaji wa sheria zisizopatia kipaumbele maslahi ya wakazi wa eneo hilo.

Haya yamejiri kufuatia Mswada unaopendekeza kubuniwa kwa Sheria kuhusu Ofisi ya Mke wa Gavana, 2023, uliowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Utumishi wa Umma na Usimamizi Kaunti hiyo na Diwani wa Wadi ya Marama, Willis Opuka.

Mswada huo unapendekeza kubuniwa kwa ofisi itakayojumuisha Mke wa Gavana na mke wa naibu gavana wakiwemo wafanyakazi walioteuliwa na Bodi ya kuajiri Watumishi wa Umma (PSC).

Endapo utapitishwa kuwa sheria, mswada huo pia unapendekezwa bajeti maalum kutengewa Ofisi ya Mke wa Gavana ikiwemo marupurupu ya wanachama wa kamati za ofisi hiyo zitakazobuniwa.

Hii ni pamoja na vipengee vingine kadhaa vinavyohusu kuepushiwa majukumu ya mtu binafsi, wafanyakazi wengine wa ofisi hiyo, usimamizi wa ofisi, hatia na taratibu husika.

Akitetea Bunge la Kaunti ya Kakamega, Diwani Opuka amehoji kuwa sheria hiyo inaambatana na Kifungu 185 (2) cha Katiba ya Kenya kinachosema “bunge la kaunti linaweza kuunda sheria zozte ambazo ni muhimu kwa, zinazohitajika, kwa utekelezaji bora wa majukumu na mamlaka ya serikali za kaunti chini ya Awamu ya Nne ya Kifungu 235 kinachozungumzia kuhusu wafanyakazi wa Serikali za Kaunti.

Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, hata hivyo, ametofautiana vikali na juhudi za kuanzisha sheria kuhusu ofisi hiyo akirejelea uamuzi uliotolewa mnamo 2015 na aliyekuwa mwanasheria mkuu Githu Muigai.

Akitoa ushauri wake kisheria, Bw Muigai alisema “wake za magavana hawapaswi kutengewa ofisi za kaunti au bajeti za kufadhili shughuli zao za uhamasishaji.”

“Ushauri huu ulitumiwa wenyekiti wa PSC, Tume ya Kufanyia Sheria Marekebisho Nchini, Tume ya Utekelezaji Katiba na Mdhibiti wa Bajeti miaka minane iliyopita. Hivyo basi haifai kamwe kwa sheria kama hiyo kujadiliwa huku ikipuuza kabisa ushauri huo,” alihoji Seneta Khalwale.

Seneti sasa imeitisha ufafanuzi kuhusu sababu ya Bunge la Kaunti ya Kakamega kupendekeza sheria hiyo licha ya uamuzi huo kuwepo na ikiwa iliomba ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kuhusu kubatilisha uamuzi huo.

Seneta Khalwale alisema haifai umma kuongezewa mzigo zaidi ikizingatiwa majukumu yaliyopendekezwa kutengewa ofisi ya mke wa gavana, tayari yanatekelezwa na ofisi zilizopo kwenye mpangilio wa usimamizi katika kaunti.

“Majukumu mengineyo yanayohusu shughuli za kutoa misaada zitakazoeneshwa na ofisi hiyo inayopendekezwa ni sawa lakini, japo ni wazo nzuri kwa wake za magavana kujihusisha na shughuli za kijamii na kutoa msaada ili kuboresha maslahi ya wanajamii katika kaunti zao, fedha za umma hazifai kutumika kufadhili shughuli hizo,” alisema.

“Kwa kuzingatia hali iliyopo nchini kwa sasa kiuchumi na kifedha, hatua ya kuanzisha ofisi ya mke wa gavana na kufadhili ofisi hiyo kutokana na fedha za umma si njia bora ya kutumia raslimali chache za umma.”

“Tunahimiza bunge za kaunti kuunda sheria kwa sababu ni moja kati ya majukumu yake makuu lakini zinapofanya hivyo ni sharti wajali maslahi ya raia. Watu wetu hawana kazi na wanaandamwa na changamoto za kifedha. Tuungane kutatua ukosefu wa ajira na matatizo mengine yanayowakabili watu wetu.”

  • Tags

You can share this post!

Seneta achemkia wanawake kwa kukataa Sh500 za motisha ya...

Al-Shabaab waua mwanamume kwa kukataa kuwaonyesha vituo vya...

T L