• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Mashirika ya kijamii yalalamikia ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela chini ya utawala wa Kenya Kwanza

Mashirika ya kijamii yalalamikia ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela chini ya utawala wa Kenya Kwanza

NA CHARLES WASONGA

MASHIRIKA ya kijamii yamelalamikia ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela chini ya utawala wa Kenya Kwanza iliyoahidi kutokomeza visa hivyo na kuhakikisha haki za kibinadamu zinaheshimiwa.

Kwenye ripoti yake kuhusu utathmini wa utendakazi wa serikali ya Rais William Ruto mwaka mmoja baada ya kuingia afisini, shirika la Independent Medico Legal Unit (IMLU) linasema kuwa visa vya mauaji ya kiholela, watu kulazimishwa kupotea na wengine kuteswa kinyama vimeandelea kushuhudiwa nchini Kenya.

Shirika hilo linasema kuwa limerekodi visa 128 vya mauaji ya kiholela kati ya Oktoba 1, 2022, hadi Agosti 31, 2023, kinyume na ahadi ya Rais Ruto ya kulinda haki za kibinadamu.

“Ndani ya muda wa mwaka mmoja uliopita, tumeshuhudia msururu wa ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha, mauaji ya kiholela, vifo vya watu kizuizini, watoto kuteswa kimakusudi, kuingiliwa kwa asasi za kuchunguza uhalifu, kuingiliwa kwa utendakazi wa polisi miongoni mwa visa vingine vya ukiukaji wa haki,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa IMLU alipotoa ripoti hiyo mnamo Alhamisi jijini Nairobi.

Akiongea katika uwanja wa michezo wa Kericho Green, mjini Kericho mnamo Oktoba 16, 2022, wakati wa ibada maalum ya shukrani, Dkt Ruto alitangaza kuvunjwa kwa kikosi maalum cha Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kilichofahamika kama Special Service Unit (SSU) ambacho kilituhumiwa kuwaua Wakenya kiholela.

Miili ya watu hao ilipatikana kando ya Mto Yala katika Kaunti ya Siaya na maeneo yenye misitu sehemu mbalimbali nchini. Baadhi ya miili hiyo ilipatikana ikiwa imekatwa vipande na kutiwa ndani ya magunia na kutupwa.

“Hiyo ni historia ambayo tunataka kusahau. Hatutaki kusikia kuwa Wakenya wanauawa kiholela na maiti zao kutupwa katika Mto Yala. Hii ndiyo maana nimeamuru kuvunjwa kwa kikosi cha SSU kwa sababu tunataka kuongoza nchi hii kwa misingi ya utawala wa sheria huku tukihakikisha kuwa haki za kibinadamu zinaheshimiwa,” Dkt Ruto akasema.

Hata hivyo, IMLU inasema tangu wakati huo, visa vya watu kupotea na maiti zao kupatikana baadaye vinaendelea kushuhudiwa nchini.

Shirika hilo linaelekeza kidole cha lawama kwa maafisa wa usalama.

Kando na mauaji ya watu 128, IMLU pia imerekodi visa vitatu vya watu kupotea wakihofia usalama wao, na visa 351 vya mateso.

Kwa ujumla, ripoti ya shirika hilo imenakili jumla ya visa 482 vya mateso na ukiukaji wa haki za kimsingi za kibinadamu.

Hii inawakilisha ongezeko la visa 250 ikilinganishwa na visa 232 vya ukiukaji wa haki vilivyorekodiwa kati ya Oktoba 1, 2022, na Agosti 31, 2023.

“Data yetu inafichua hali ya kuogofya kutoka Oktoba 1, 2022, hadi Agosti 31, 2023. Tulinakili jumla ya visa 482 vya mateso na ukiukaji wa haki za kibinadamu. Idadi hii ni zaidi ya maradufu ya visa vilivyonakiliwa katika kipindi sawa na hicho kati ya miaka ya 2021 na 2022.

Matokeo ya uchunguzi wa IMLU yanaonyesha kuwa wengi wa wahasiriwa ni wanaume wenye umri mdogo wa kati ya miaka 18 na 35, idadi ikiwa ni jumla ya watu 314.  Wanafuatwa na watu wenye umri wa kati ya miaka 36 na 65, ambao ni jumla ya watu 121.

Wale wenye umri wa miaka 17 kwenda chini walikuwa 44 na watatu walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 65.

Kati ya waathiriwa hao 482 jumla ya 67 walikuwa ni wanawake.

Huku akilalamika kuwa wengi wa wahasiriwa ni vijana, wanaowakilisha asilimia 65 ya idadi jumla, Bw Kiama amemkashifu Rais Ruto kwa kutotimiza ahadi yake ya kulinda vijana dhidi ya ukatili wa polisi.

Shutuma za IMLU zinajiri saa chache baada ya Tume ya Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC), Katiba Institute, shirika la Transparency International-Kenya na ICJ-Kenya kudai mwaka wa kwanza wa utawala wa Kenya Kwanza umeshuhudia visa vya watu kukamatwa kiholela na mauaji.

Watetezi hao wa haki za kibinadamu pia walisema kuwa wao wenyewe pia wamekuwa wakipokea vitisho dhidi ya maisha yao katika jaribio la kuwanyamazisha.

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro aagiza daktari anayedaiwa kulewa kazini apelekwe...

Bungoma Queens waingia sokoni kusaka majembe kabla ya msimu...

T L