• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Mbunge apendekeza CEO wa IEBC apewe mamlaka ya mwenyekiti wa tume

Mbunge apendekeza CEO wa IEBC apewe mamlaka ya mwenyekiti wa tume

NA CHARLES WASONGA

AFISA Mkuu mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) atasimamia chaguzi ndogo za maeneobunge na wadi ikiwa mswada uliodhaminiwa na Mbunge wa Mandera Kaskazini, Abdullahi Bashir utapitishwa kuwa sheria.

Mbunge huyo Jumatano, Desemba 6, 2023 ametoa vidokezo kuhusu mswada huo ambao anasema unalenga kusuluhisha dosari iliyoko katika Sheria ya IEBC ya 2012.

Kulingana na sheria hii inayotumika sasa, ni mwenyekiti wa tume hiyo, akisaidiwa na angalau makamishna wawili, walio na mamlaka ya kuendesha chaguzi ndogo za maeneo hayo wakilishi baada ya nafasi hizo kusalia wazi.

“Dhima ya mswada wangu ni kumpa afisa mwenye cheo cha juu zaidi katika IEBC mamlaka ya mwenyekiti kiasi kwamba anaweza kuteua afisa wa kusimamia chaguzi ndogo endapo itatokea kwamba makamishna hawapo,” Bw Bashir akasema wakati wa kikao cha Bunge la Kitaifa cha alasiri.

Alisema mswada wake unalenga kuifanyia mageuzi sehemu ya 18 ya Sheria ya IEBC ya 2012 inayosema kuwa ni mwenyekiti wa tume hiyo pekee aliye na mamlaka ya kuteua afisa wa kusimamia uchaguzi mdogo katika eneo lolote wakilishi.

“Ingawa Katiba inasema kuwa kila Mkenya ana haki kupata uwakilisha bunge au eneo lolote wakilishi hadi kufikia sasa wakazi wa maeneobunge ya Banisa na Magarini hawana mwakilishi katika bunge hili. Zaidi ya wadi 20 ziko wazi baada ya madiwani kufariki au mahakama kubatilisha ushindi wao katika uchaguzi mkuu wa 2022. Hii sio haki na dosari hii inapaswa kurekebishwa licha ya kwamba IEBC haina makamishna wakati huu,” Bw Bashir akasema.

Kiti cha ubunge cha Banisa kilisalia wazi baada ya kifo cha mbunge Hassan Maalin Hassan mnamo Machi 29, 2023. Kiongozi huyo alikata roho akitibiwa katiika hospitali ya Mater, Nairobi baada ya kugongwa na mwendeshaji bodaboda akivuka barabara kuelekea katika msikiti mtaani South B, Nairobi.

Nacho kiti cha ubunge cha Magarini, kilibaki wazi baada ya mahakama kuu kubatilisha ushindi wa Harrison Garama Kombe katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mahakama Kuu ya Malindi ilibatilisha ushindi wake Mei 26, 2023 baada kugundua dosari katika uhesabu wa kura.

 

  • Tags

You can share this post!

Wadudu wa ‘Nairobi fly’ wanavyohangaisha Wakenya msimu...

Wizi wa pikipiki wazidi wahudumu wakiuawa

T L