• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Mbunge Owen Baya aanza kulainisha sekta za kilimo cha minazi na korosho akifufua matumaini ya wengi waliokuwa wamekata tamaa

Mbunge Owen Baya aanza kulainisha sekta za kilimo cha minazi na korosho akifufua matumaini ya wengi waliokuwa wamekata tamaa

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wameunga mkono mpango wa kufufuliwa kwa sekta za kilimo cha minazi na korosho katika eneo la pwani kurejesha fahari ya zamani.

Wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Kilimo wamefanya hivyo kwa kuunga mkono Mswada wa Nazi na Korosho wa 2023 unaodhaminiwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya.

Mswada huo kielelezo unapendekeza sheria mpya itakayosimamia ukuzaji, usindikaji, uhifadhi, usafirishaji na uuzaji wa bidhaa za minazi na korosho.

Mbunge wa Sigowet/Soin Justice Kipsang Kemei (kushoto) na Mbunge wa Konoin Brighton Yegon, ambaye ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo, wakiwa katika ukumbi wa County Hall, Majengo ya Bunge jijini Nairobi wakati wa kikao cha kamati hiyo cha kujadili Mswada wa Nazi na Korosho wa 2023. Mswada huo umedhaminiwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya. PICHA | CHARLES WASONGA

Aidha, mswada huo unapendekeza kuundwe kwa Bodi ya Minazi na Korosho Nchini itayosimamia utekelezaji wa sheria kuhusu ukuzaji, uhifadhi, uuzaji, utafiti na ustawishaji wa minazi na korosho.

Akiunga mkono mswada huo, Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Lamu Monica Marubu alisema ipo haja ya sekta hizo kufufuliwa kwa sababu kuna soko kubwa zaidi la bidhaa zinazotengenezwa kutokana na nazi na korosho nchini na hata mataifa ya nje.

Alisema kuwa sekta hizo zimefifia kwa sababu wakulima wamekosa kupewa motisha kufanikisha kilimo cha mazao hayo na hali kwamba aina ya minazi inayokuzwa pwani ni ile inayokomaa kwa miaka mingi.

“Tunafaa kutambua umuhimu wa mazao haya mawili lakini inasikitisha kuwa kilimo chao kinafifia. Ikiwa tunaweza kupata asasi itakayolenga kusimamia minazi na korosho, tunaweza kufufua sekta hizo. Hali ya anga katika eneo la pwani ni bora kwa kilimo cha mazao hayo. Ninapendekeza kamati hii iidhinishe mswada huu kutokana na umuhimu wake,” akasema mnamo Jumanne katika majengo ya bunge, wakati wa kikao cha kamati hiyo ya kupiga msasa mswada huo.

Mbunge wa Kwanza Ferdinand Wanyonyi alieleza matumaini kuwa kufufuliwa kwa sekta hizi kutainua uchumi wa eneo la pwani.

“Kilimo cha minazi kinafifia ilhali tunaihitaji. Tunafaa kuunga huu mswada wa Bw Baya ili kufufua sekta hii kwa manufaa ya wakazi wa eneo la pwani na Kenya kwa ujumla,”akasema Bw Wanyonyi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Borabu Patrick Osero alipendekeza kufutiliwa mbali kwa Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA), akisema asasi hiyo haiwasaidii wakulima.

“Japo sekta za minazi na korosho zimewekwa chini ya AFA, asasi hii haifanya lolote kufufua sekta hizi. Hii ndiyo maana wazo la kubuniwa kwa bodi mahsusi ya kusimamia sekta hizi ni muhimu zaidi,” akasema mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa kwanza.

Mbunge wa Borabu Patrick Osero (kushoto) na Mbunge Mwakilishi wa Lamu Monica Marubu. Hawa ni miongoni mwa wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo wanaounga mkono mswada wa Bw Baya unaolenga kufufua sekta za kilimo cha Minazi na Korosho. PICHA | CHARLES WASONGA

Licha ya wabunge kuunga mkono mswada huo, Wizara ya Kilimo na Ustawi wa Mifugo imeupinga.

Kwenye taarifa iliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo ya bunge kuhusu Kilimo, Wizara hiyo inasema kuwa malengo ya Mswada wa Nazi na Korosho yanashughulikiwa na Sheria ya Mimea ya 2013, Sheria ya AFA ya 2013 na Kanuni kuhusu Mazao yanayozalisha Mafuta ya 2020.

Hata hivyo, Tume kuhusu Mageuzi ya Sheria iliunga mkono mswada huo ambao sasa unasubiri kuchapishwa rasmi kabla ya kuwasilishwa kwa kamati ya bunge lote kujadiliwa.

Kwa miaka mingi kilimo cha minazi na korosho kimekuwa kitega uchumi kwa wakazi wa kaunti za Kwale, Kilifi, Tana River, Mombasa, na Lamu.

Lakini mnamo 1997 Kiwanda cha Korosho Nchini kilisambaratika kutokana na usimamizi mbaya licha ya kwamba kilikuwa na uwezo wa kusindika jumla ya tani 15,000 za zao hilo kila mwaka.

Mnamo Juni 2022, Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo ilishughulikia ombo kutoka kwa baadhi ya wakazi wa pwani walioitaka serikali ifufue kiwanda hicho.

  • Tags

You can share this post!

Aliyepandikizwa nywele husubiri kati ya mwaka mmoja na...

EACC yaenda Bomas kuomba meno

T L