• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Mchango wa Shakahola kwa vita vya uhuru wa Kenya

Mchango wa Shakahola kwa vita vya uhuru wa Kenya

NA MAUREEN ONGALA

WAKATI Kenya inasherehekea sikukuu ya Madaraka Dei, jamii ya Wamijikenda inaendelea kukumbuka mchango wa msitu wa Shakahola kwa vita vya ukombozi wa nchi kutoka kwa wakoloni.

Msitu huo ulio katika eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, kwa miezi kadha sasa umezoa sifa mbaya ya mauaji ya halaiki ya watu wanaoaminika walikuwa waumini wa dhehebu linalohusishwa na mhubiri Paul Mackenzie, ambaye yuko kizuizini.

Hata hivyo, katika historia ya Wamijikenda, ni katika msitu huo ambapo mpiganaji mashuhuri wa uhuru, Mekatilili wa Menza, anasemekana alimzaba kofi mkoloni Mwingereza.

“Mau Mau walitambua msitu wa Shakahola kama mojawapo ya ngome zilizochangia kwa uhuru wa Kenya, lakini sasa tutahifadhi historia nyingine ya kuambia vizazi vijavyo kuhusu mhubiri na mafunzo yake tatanishi ambayo yaligeuza msitu huo kuwa makaburi,” akasema Mwenyekiti wa Muungano wa Utamaduni wa Wilaya ya Malindi, Mzee Emmanuel Munyanya.

Mekatilili wa Menza pia anakumbukwa kwa unabii wake kuhusu kuja kwa watu wa ajabu “wenye nyuzi za mkonge zinazofanana na hewa ambao walisafiri kwenye vyombo vya kuruka angani, juu ya maji na nchi kavu”, kumaanisha wakoloni.

Shujaa huyo alipinga kazi ya kulazimishiwa vijana wa jamii ya Wagiriama na ushuru uliokandamiza wenyeji.

Wazee wa Kaya za Mijikenda walisema wataendelea kuhifadhi msitu wa Shakahola kama eneo la kihistoria.

“Baada ya operesheni za kuondoa miili kutoka kwenye makaburi msituni, tunataka msitu wa Shakahola ulindwe kama eneo la kihistoria chini ya wazee wa Kaya. Hakuna mtu atakayeruhusiwa kumiliki ardhi,” akasema Mratibu wa Jumuiya hiyo, Bw Tsuma Nzai.

Mratibu huyo alisema wataweka mnara kuashiria mahali ambapo Mekatilili wa Menza alimzaba kofi mkoloni wa Uingereza.

Marehemu Mekatilili wa Menza alizikwa katika kijiji cha Ulaya Kwa Jele huko Bungale, mwaka 1924 baada ya kuwaongoza Wagiriama dhidi ya wakoloni Waingereza.

Jamii ya Wamijikenda huadhimisha kumbukumbu za Mekatilili wa Menza kila mwaka mwezi wa Agosti kwa siku tatu kando ya kaburi lake Bungale.

Msitu wa Shakahola ni sehemu ya shamba kubwa la Chakama ambapo kuna wakazi wanaofanya kilimo.

  • Tags

You can share this post!

Maadhimisho ya Madaraka Dei Juni 1, 2023, katika Uwanja wa...

Moraa aamua kushiriki riadha za polisi badala ya Diamond...

T L