• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Meneja afafanua ndege ilipata panchari ikitua uwanjani Manda

Meneja afafanua ndege ilipata panchari ikitua uwanjani Manda

NA KALUME KAZUNGU

SHUGHULI zilitatizika kwa muda katika uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu Jumatatu jioni pale ndege ya kibinafsi iliyokuwa ikitua uwanjani humo ilipata panchari.

Ndege hiyo ya kibinafsi ya kampuni ya Scenic Air Safaris ilisababisha kucheleweshwa kwa safari za ndege nyingine zilizofaa kutua na kupaa kutoka uwanjani humo majira ya saa kumi alasiri.

Akithibitisha tukio hilo, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Manda Bw Felix Wanga, amesema Mamlaka ya Usimamizi Wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) ililazimika kuzielekeza ndege zilizofaa kutua kwa wakati huo hadi uwanja wa ndege wa Malindi, Kaunti ya Kilifi ambapo zilitua kwa muda kwa sababu ya kuzingatia usalama wa abiria waliokuwa ndegeni.

Bw Wanga aidha aliwasihi wasafiri na wananchi kuwa watulivu wakati KAA ikifanya jitihada kurekebisha tatizo hilo.

“Ni kweli kumekuwa na ndege ya kibinafsi iliyokuwa ikitua uwanjani Manda hivi jioni. Ilipata panchari ya gurudumu lake hivyo kukwama katikati ya uwanja. Uwanja wetu nafasi yake tayari haitoshi, hivyo haiwezekani kuruhusu ndege kutua au kupaa wakati ile iliyoharibika ikiwa uwanjani. Tumefanya mawasiliano ya haraka, ambapo ndege mbili zilizofaa kutua uwanjani Manda hivi jioni tumezielekeza kwenye uwanja wa ndege wa Malindi ambapo zitatua kwa muda wakati tukishughulikia Na kutatua tatizo lililopo. Watu wasiwe na Shaka,” akasema Bw Wanga.

Tukio la kupasuka kwa gurudumu la ndege na kuikwamisha katikati ya uwanja wa ndege wa Manda limesababisha kucheleweshwa kwa safari za baadhi ya wasafiri,hasa wale waliokuwa tayari kuondoka uwanjani Manda kuelekea Nairobi na Malindi na pia wale waliokuwa wakija Lamu kutoka Nairobi.

Baadhi ya abiria waliohojiwa na Taifa Leo na kudinda kutaja majina walieleza kusikitishwa kwao na tukio hilo, wakiisihi KAA kufanya hima kutatua tatizo hilo na kuruhusu safari zao kuendelea.

“Haturidhishwi kamwe na mipangilio ya uwanja huu. Kama ndege imepata panchari na kukwama uwanjani,kwa nini isiburutwe Na kuwekwa kando ili kuruhusu shughuli za kawaida kuendelea uwanjani hapa. Wengine tunalazimika kukatiza mipango yetu kutokana na kucheleweshwa kwa safari na hatuoni dalili ya ni lini tatizo litatatuliwa. Hii si haki kamwe,” akasema mmoja wa maabiria.

Miongoni mwa walioathiriwa na panchari ya ndege na safari zao kucheleweshwa ni watalii ambao tayari walikuwa wamekwama hotelini Lamu tangu Jumamosi pale mafuriko yaliposomba eneo la Gamba, kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, hivyo kukatiza usafiri wa barabarani.

Ndege iliyopata panchari ilikuwa imefikishwa Lamu kuwachukua watalii hao.

“Hiki ni kisirani. Mafuriko yalitulazimu kukaa Lamu siku ya pili sasa tangu tamasha za utamaduni wa Lamu kukamilika Jumamosi usiku. Tulitarajia kufika Malindi Na Nairobi mapema lakini kisirani cha panchari nacho ndicho hiki,” akasema mmoja wa wasafiri aliyedinda kutaja jina.

Si mara ya kwanza kwa ndege kukwama uwanjani Manda,kaunti ya Lamu na kupelekea safari za abiria kucheleweshwa.

Mnamo Septemba 2023, ndege ya kampuni ya Jambo Jet ilikwama kwenye shimo uwanjani Manda wakati ikipaa.

Hali hiyo ilizua taharuki miongoni mwa abiria waliokuwa ndani,wengine wakitaka kirika kutoka ndegeni.

Hata hivyo hakuna abiria aliyejeruhiwa wakati wa tukio hilo.

  • Tags

You can share this post!

Jamaa wa wanaume sita walioshtakiwa kwa wizi wa Sh94...

COP28: Kenya kupokea kima cha Sh1.5 bilioni kuangazia...

T L