• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 12:33 PM
Mfuasi sugu wa Azimio ashtakiwa kumdhalilisha Rais Ruto

Mfuasi sugu wa Azimio ashtakiwa kumdhalilisha Rais Ruto

Na RICHARD MUNGUTI

HATIMAYE mfuasi sugu wa kinara wa Azimio Raila Odinga, Nuru Maloba Okanga amefichua alikuwa amepata alama 320 katika mtihani wa Darasa la Nane.

Bw Okanga mwenye umri wa miaka 32, alifichulia wakili Emmanuel Kibeti katika Mahakama ya Milimani aliposhtakiwa kwa kumdhalilisha Rais William Ruto siku 10 zilizopita.

Bw Okanga ambaye ameoa na amejaaliwa watoto watatu amekuwa akikwepa kusema alama alizopata katika mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) ambao matokeo yake yalitangazwa Novemba 23, 2023 na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Akijibu maswali ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Lucas Onyina, Bw Okanga alifichua alifanya mtihani wa KCPE katika Shule ya Msingi ya Mumias Muslim iliyoko Kaunti ya Kakamega.

“Ulisoma katika shule gani?” hakimu alimuuliza mshtakiwa.

“Mumias Muslim Primary School,” Bw Okanga alijibu.

“Umeteuliwa kujiunga na shule ipi ya Sekondari,” Bw Onyina alimhoji zaidi.

“Bado sijapokea barua ya mwaliko kujiunga na Kidato cha Kwanza. Uteuzi haujafanywa,” Bw Okanga alijibu.

Baada ya kujibu maswali hayo ya hakimu mshtakiwa aliyekuwa ametiwa pingu mkono mmoja aliondoka kizimbani na kujiunga na mahabusu wengine.

Wakili wake Bw Emmanuel Kibeti alimsongelea kizimbani na kumuuliza “ulizoa alama gapi katika mtihani wa KCPE?”

“Nilipata alama 320,” Bw Okanga alimweleza Bw Kibet.

Mwanafunzi huyo aliyehitimu 2023 alikabiliwa na shtaka la kumdhalilisha Rais Ruto.

Bw Okanga alishtakiwa kwa kumtusi Rais Ruto maneno ambayo hatuwezi chapisha kwa sababu ya sheria za kudhibiti uanahabari.

Bw Okanga alishtakiwa kumkejeli Rais Ruto kupitia mtandao wake wa YouTube unaojulikana kwa jina Riba News @ribanews.

Habari hizo zenye matusi hayo zilikuwa chini ya kichwa “Nuru Okanga On Fire.”

Shtaka lilisema Bw Okanga alinakili matusi hayo kwenye video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Bw Okanga amedaiwa matamshi yake katika video hiyo ni ya uwongo na hayana msingi na kwamba alilenga kuudhi afisa wa serikali na kuvuruga amani.

Bw Kibet aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana akisema “ni mkazi wa Riverside Nairobi na hawezi kutoroka.”

“Naomba hii mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana. Alimaliza Darasa la Nane mwaka huu na anasubiri kujiunga na Kidato cha Kwanza. Hawezi kutoroka,” Bw Kibet alimweleza hakimu.

Akitoa uamuzi Bw Onyina alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh10,000 pesa tasilimu.

Alitenga kesi hiyo itajwe tena Desemba 13, 2023 itengewe siku ya kusikizwa.

Pia mahakama iliamuru apewe nakala za mashahidi aandae tetezi zake.

Mshtakiwa alitiwa nguvuni Novemba 29, 2023 na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Capitol Hill usiku kucha.

Alikifikishwa kortini Novemba 30, 2023.

Baadhi ya mashahidi walioorodheshwa ni pamoja na maafisa watatu wa polisi Konstebo Morgan Wekesa, Inspekta Mkuu John Kahonge na Inspekta Mkuu Nickson Kinyua.

  • Tags

You can share this post!

Ajuza wa miaka 70 akaidi sayansi na kujifungua mapacha

Wakuzaji mpunga wapinga kubinafsishwa kiwanda cha Mwea

T L