• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:30 PM
Mhubiri atupwa ndani kwa kupatikana na chang’aa

Mhubiri atupwa ndani kwa kupatikana na chang’aa

NA TITUS OMINDE

MCHUNGAJI mmoja maarufu kutoka mji wa Moi’s Bridge aliyepatikana na pombe haramu amefikishwa mbele ya Mahakama ya Eldoret.

Mchungaji Isaac Tenge alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Rosemary Onkoba.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Septemba 24, 2023, alipatikana akiwa na lita 70 za chang’aa nyumbani kwake Moi’s Bridge katika kaunti ndogo ya Soy, Kaunti ya Uasin Gishu.

Mchungaji Tenge alikana shtaka hilo na mahakama ikaamuru aachiliwe kwa bondi ya Sh100,000 au dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu.

Hata hivyo, mtumishi huyo wa Mungu alishindwa kulipa dhamana huku akiiomba mahakama impunguzie angalau hadi Sh5,000 akidai kuwa kwa sasa kanisa hilo halifanyi vizuri kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili waumini.

Nakala za kesi hiyo zinaonyesha kuwa yeye ni mchungaji wa kanisa la New Jerusalem katika mji wa Moi’s Bridge.

Kinaya ni kwamba hakuna hata mmoja wa washirika wa kanisa hilo aliyefika mahakamani kusimama na mchungaji wao ila mkewe na wanawe wawili na binti mmoja.

Baada ya kushindwa kulipa dhamana alizuiliwa katika gereza la Eldoret.

Hapo awali, pasta huyo aliambia mahakama kuwa maafisa wa polisi walimjeruhi mwilini wakati wa kumkamata hivyo basi alitaka agizo la kupelekwa hospitlaini kwa matibabu.

“Polisi walimpiga mke wangu na kumjeruhi mikono vibaya kabla ya kunigeukia na kunipiga mkono wa kulia, ambao una majeraha mabaya. Ninahitaji matibabu ya haraka,” akaomba pasta.

Hakimu alimhakikishia mhubiri huyo kuwa mvumilivu akibainisha kuwa malalamiko yake yatashughulikiwa na wakili wa serikali.

Mchungaji alikana shtaka hilo.

Alikamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Moi’s Bridge kufuatia msako mkali wa kutokomeza pombe haramu katika eneo hilo.

Maafisa hao walivamia nyumba yake kufuatia taarifa kutoka kwa wananchi na kuchukua pombe hiyo haramu.

Tukio hilo liliwaccha wafuasi wengi wa kanisa hilo na mshangao.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 5.

  • Tags

You can share this post!

Warembo wa Kiislamu Lamu wataja sababu za kudinda kuolewa

SHINA LA UHAI: Ongezeko la taka za kielektroniki tishio kwa...

T L