NA BRIAN OCHARO
MHUBIRI Ezekiel Odero ameelekea mahakamani tena kuomba agizo la kufungwa kwa akaunti zake za benki na zile za kanisa lake la New Life Prayer Centre and Church lifutiliwe mbali.
Katika stakabadhi zake alizowasilisha mbele ya Mahakama Kuu ya Mombasa, Jumanne, Ezekiel, ambaye anachunguzwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo mauaji ya halaiki, amekashifu serikali kwa kumdhulumu kwa makosa ambayo si yake.
“Naomba mahakama hii itoe amri ya kufutilia mbali kwa muda agizo la mahakama ya mahakimu ya kufungia akaunti zangu za benki,” amesema
Pia, Mhubiri huyo ameomba Jaji wa Mahakama ya Mombasa Olga Sewe kusimamisha kwa muda utekelezaji wa maagizo ya mahakama ya Milimani na kesi zote zinazofanyika katika mahakama hiyo kuhusiana na mali yake.
Kupitia kwa mawakili wake wakiongozwa na Danstan Omari, Jared Magolo, Cliff Ombeta na Danstan Omari, Mhubiri huyo pia anataka Jaji Sewe atoe amri ya kuzuia Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na mashirika mengine ya serikali ili yakome kuchunguza mali yake.
Pia, anataka Mahakama Kuu kufutilia mbali maagizo yaliyotolewa mnamo Mei 8, 2023 yanayoruhusu kufungwa kwa akaunti 35 za benki na Mpesa zilizosajiliwa kwa jina lake na la kanisa lake.
Mhubiri Ezekiel pia amelalamika kuwa kufungiwa kwa akaunti zake za benki kutaathiri vibaya elimu ya wanafunzi zaidi ya 3800 wanaotegemea mpango wake wa ufadhili.
“Shule zimefunguliwa na hakuna pesa za kuwalipia wanafunzi hao karo. Serikali sasa inaweza kuchukua jukumu hilo,” amesema Danstan Omari.
Mahakama ya Milimani jana Jumatatu ilitoa amri ya kufungia akaunti 35 za benki baada ya DCI kusema kuwa inamchunguza mwinjilisti huyo kwa utakatishaji fedha.
Mahakama pia iliruhusu Kitengo cha Uchunguzi wa Kifedha cha DCI kuchunguza akaunti za benki zikiwemo akaunti za Mpesa za mwinjilisti huyo , kanisa lake na shule ya Kilifi International.
Inspekta wa polisi Martin Munene alisema akaunti za benki za Mhubiri Ezekiel zimekuwa zikipokea bunde la fedha.
Kulingana na DCI, fedha hizo zinashukiwa kuwa sehemu ya mapato ya pesa haramu kutoka kwa waathiriwa wa mauji ya Shakahola ambao wanasemekana kuuza mali yao na kumpa kiongozi wao Paul Mackenie.
Mackenzie pia anachunguzwa kwa makossa kadhaa yakiwemo mauji ya halaili ya watu, utakatishaji fedha na hitikadi kali kutokana na maujai ya halaiki ya watu katika eneo la Shakahola.
Hata hivyo, mawakili wa Bw Ezekiel wakiongozwa na Jared Magolo, Cliff Ombeta, Bw Omari na Shadrack Wambui wameshutumu serikali kwa kumdhulumu kwa kumhusisha isivyo haki na Mackenzie.
Mawakili hao walilalamikia Jaji Sewe kwamba swali na suala la kufungia akaunti ya mteja wao tayari lilikuwa chini ya ombi lililo mbele ya mahakama yake na lilikuwa likisubiri kusikilizwa na kuamuliwa.
Mchungaji Ezekiel anachunguzwa kwa makosa ya, kusaidia kujiua, mauaji, utekaji nyara, itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukatili wa watoto na ulaghai.