• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Mkenya aliyetaka TikTok izimwe sasa alegeza msimamo

Mkenya aliyetaka TikTok izimwe sasa alegeza msimamo

NA CHARLES WASONGA

MLALAMISHI aliyetaka mtandao wa TikTok upigwe marufuku nchini kwa kueneza taarifa na picha chafu amelegeza pendekezo lake na sasa anataka sheria kali iwekwe kudhibiti matumizi ya mtandao huo wa kijamii.

Bw Bob Ndolo, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ushauri la Bridget Connect Consultancy, amelifanyia marekebisho ombi lake ili kulenga udhibiti baada ya kupokea rai kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu matumizi ya apu hiyo.

Mlalamishi huyo alisema hayo Jumanne, Septemba 26, 2023, alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Kushughulikia Malalamishi kutoka kwa Umma katika Majengo ya Bunge jijini Nairobi.

Kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai, ilitwikwa wajibu wa kushughulikia ombi hilo ambalo Bw Ndolo aliwasilisha katika Bunge la Kitaifa mnamo Agosti 15, 2023.

Lakini pendekezo la Bw Ndolo kwamba TikTok ipigwe marufuku Kenya lilipata pingamizi kubwa kutoka kwa wabunge wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na mwenzake wa mrengo wa wachache Opiyo Wandayi.

Wabunge hao walisema kuwa Wakenya wengi, haswa vijana, huchuma mapato kupitia apu hiyo iliyoasisiwa nchini China kwa kuweka maudhui hayo humo.

Walipendekeza kuwa badala ya kupigwa marufuku kwa TikTok, sheria iwekwe ya kuadhibu wanaotumia jukwaa hilo vibaya kwa kusambaza taarifa na picha chafu.

Ni baada ya suala hilo kuibua hisia mseto nchini ambapo Rais William Ruto alifanya kikao na Afisa Mkuu Mtendaji wa TikTok Shou Zi Chew. Walikubaliana kuhusu njia za kuimarisha usimamizi wa mtandao huo ili kuwazima watu ambao huitumia kusambaza mambo machafu.

Hii ndio maana Bw Ndolo alipofika mbele ya Kamati ya Bw Mbai mnamo Jumanne, alisema hivi: “Tumekuwa tukipokea simu kutoka kwa watumiaji wengi wa TikTok. Hii ndiyo maana tumelegeza msimamo na kuamua kushinikiza kuwa apu hiyo isimamiwe kisheria ili kuzuia athari za matumizi yake kwa usalama wa kitaifa na kuzuia watoto wetu kutokana na athari za mambo mabaya yanayosambazwa kupitia mtandao huo.”

Bw Ndolo alisisitiza kuwa hakutishwa kulifanyia mabadiliko ombi lake la awali kwamba TikTok ipigwe marufuku, haswa baada ya Rais Ruto kukutana na uongozi wa TikTok.

“Tunafahamu kuwa Rais alifanya majadiliano na Afisa Mkuu wa TikTok ila tulipata habari hiyo kupitia vyombo vya habari. Hatukuhusishwa kwa njia yoyote. Tulikutana tu na usimamizi wa TikTok kutoka Afrika Kusini. Hatujapokea simu yoyote kutoka kwa Ikulu,” Bw Ndolo akaambia wabunge wanachama wa kamati hiyo.

Wakili wa shirika la Bridget Connect Consultancy, Collins Osewe, alisema kuwa apu ya TikTok imevunja Katiba na sheria mbalimbali huku akitoa wito kwa watu kuchujwa kabla ya kuruhusiwa kujiunga na mtandao huo.

“Sheria ya kusimamia matumizi ya mtandao huu wa kijamii kuzuia usambazaji wa taarifa na picha chafu inahitajika na inafaa kusema kuwa wanachama wa mtandao huu wawe watu wa tabaka na sifa fulani pekee. Usiwe mtandao wa kutumika na kila mtu,” akasema Bw Osewe.

  • Tags

You can share this post!

Sponsa ananipa kila kitu na sasa anataka nimzalie mtoto,...

Wafanyakazi wa kampuni ya maji wadai haki baada ya mwenzao...

T L