• Nairobi
  • Last Updated February 23rd, 2024 12:48 PM
Mkongwe kutembea kilomita 300 kuadhimisha Madaraka Dei 2023 Embu     

Mkongwe kutembea kilomita 300 kuadhimisha Madaraka Dei 2023 Embu    

NA MERCY KOSKEI

MZEE wa miaka 69 kutoka Kaunti ya Nakuru amewashangaza wengi baada ya kufunga safari kwa miguu ili kuhudhuria sherehe ya Madaraka 2023, itakayoadhimishwa Kaunti ya Embu juma lijalo.

Kulingana na Stephen Muigai, mkaazi wa Bondeni, hatua ya kufunga safari wiki moja kabla ya sherehe hiyo ya kitaifa inaashiria uzalendo wake kwa taifa na pia kuenzi waliopigania uhuru.

Akihutubia wanahabari mnamo Alhamisi, Mei 25, 2023, Mzee Muigai alisema kuwa atatembea kwa zaidi ya kilomita 300 hadi Embu huku akitarajia kuwa atapata fursa ya kukutana na mashujaa wengine.

“Nimejitolea kutembea kwa miguu kwa ajili ya sherehe hii, napenda nchi yangu ya Kenya kwa dhati, na pia nitakuwa nawaenzi waliopigania uhuru wetu.

“Ningeomba Wakenya wenzangu wajitolee na kufika. Hii itakuwa sherehe ya kwanza ya madaraka kwa Rais wetu William Ruto,” alisema Bw Muigai.

Rais Ruto ataongoza taifa katika kuadhimisha sherehe hiyo.

Muigai alifichua kuwa hii itakuwa mara yake ya saba kutembea kwa minajili ya kuhudhuria sherehe mbalimbali za kitaifa katika kaunti tofauti, ikiwemo Kakamega, Kirinyaga na Nairobi.

Mkenya huyo pia alisema kuwa alikuwa miongoni mwa walioudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Ruto 2022 katika Uwanja wa Kasarani, Nairobi akieleza kuwa alikuwa wa kwanza kufika kwa sababu ya upendo wake kwa nchi  yake.

  • Tags

You can share this post!

Babu Owino aorodheshwa mbunge bora zaidi katika utendakazi

Kenya Kwanza yarai Azimio kurejelea mazungumzo

T L